MWENDA AWATAKA WANANCHI KUTUNZA MAJENGO YA MAHAKAMA

Na Charles Kikoricho 



Mheshimiwa Ayubu Yusuph Mwenda Jaji Mfawadhi Mahakama kuu ya Tanzania Masijala Ndogo Singida amewataka wananchi kutunza majengo mapya ya mahakama ili yaendelee kudumu na kutoa huduma kwa muda mrefu, huku akiwasisitiza watumishi wa mahakama kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa.



Jaji Mwenda ametoa kauli hiyo leo tarehe 22/6/2026 wakati wa uzinduzi wa Mahakama za Mwanzo za Mungumaji  Wilaya ya Singida na Minyughe wilaya ya Ikungi Pia  ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa majengo mapya na ukarabati wa majengo ya mahakama, hatua inayolenga kuboresha utoaji wa haki nchini.



Kwa upande wake, Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Singida, Aloyce Masua, amesema mahakama hizo mbili zitarahisisha upatikanaji wa huduma za mahakama kwa wananchi na kupunguza gharama walizokuwa wakitumia kufuata huduma katika maeneo ya mbali.


Naye Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mungumaji, Modesta Mshana, amesema mahakama hiyo itahudumia wananchi wa kata za Misuna, Unyamikumbu, Kisaki na Kindai pamoja na maeneo ya jirani. Ameongeza kuwa uwepo wa mahakama hiyo utasaidia wananchi kupata haki kwa wakati na kujifunza masuala mbalimbali ya kisheria.



Kwa upande wake, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Minyughe Dogratius Haule, amesema mahakama hiyo itawahudumia wananchi wa kata za Mtunduru na  Ighombwe na  kuwaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za mahakama.



Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wameishukuru Serikali kwa kuwasogezea karibu huduma za mahakama, wakisema hatua hiyo itapunguza muda na gharama za kupata huduma za haki.

Mwisho

Post a Comment

Previous Post Next Post