Na Mwandishi Wetu, Manyoni
Kesi ya Uhujumu Uchumi Na. 13485/2026 imefunguliwa Juni 16, 2026 katika Mahakama ya Wilaya ya Manyoni dhidi ya watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni: Aliyekuwa Mweka Hazina Bw. George Mzeru, na Maafisa Mahesabu ambao ni Bw. Emilian Mauki, Bw. Lutufyo Mwakapala, Bw. Edward Kilumbu, Bi. Revania Ruheta, Bi. Doreen Shirima, Bw. Salum Mafita na Mzabuni wa ML Kimboka General Trading; Bw. Michael Mushi.
Washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka sita ambayo ni Utakatishaji Fedha kinyume na kifungu cha 12 (1) (d), na 13 (1) (a) vya Sheria ya Kuzuia Utakatishaji Fedha Sura ya 423 Marejeo ya 2023, Kuongoza Genge la Uhalifu kinyume na Aya 4 (1) na Kuisababishia Mamlaka Husika Hasara kinyume na Aya ya 10 (1) za jedwali la kwanza na kifungu cha 57(1) na (2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa Sura ya 200 Marejeo ya 2023, Wizi wakiwa Watumishi wa Umma kinyume na kifungu cha 258 (1) na 270 vya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 Marejeo ya 2023, Ufujaji na Ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 (1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Sura ya 329 Marejeo ya 2023.
Inadaiwa kuwa katika kipindi cha Julai 01, 2024 hadi Mei 29, 2026, washtakiwa walitenda makosa hayo na kusababisha hasara kwa Serikali.
Mashtaka yalisomwa na Wakili wa Serikali Bw. Godfrey Songolo mbele ya Mheshimiwa Ailisile Mwankejela Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni. Washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote, hata hivyo wamekosa dhamana kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana.
Kesi imeahirishwa hadi *Juni 30, 2026* kwa ajili ya kutajwa kwa kuwa uchunguzi bado unaendelea.



Post a Comment