Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
JUMLA ya ajira 15,764 zimezalishwa na biashara 9,020 kuanzishwa katika Mkoa wa Singida kupitia jitihada za Shirika lisilo la Kiserikali la Hand in Hand Eastern Africa Tanzania katika kukabiliana na tatizo la umaskini nchini.
Meneja wa shirika hilo Mkoa wa Singida, Glory Temu, alieleza hayo juzi wakati wa Jukwaa la Uunganishaji wa Masoko (Market Linkage Forum) lililowakutanisha wadau wa sekta ya ufugaji wa kuku.
Alisema jukwaa hilo linalenga kuwajengea wanufaika fursa za masoko na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya wazalishaji na wanunuzi wa mazao yatokanayo na ufugaji wa kuku.
Temu alisema mbali na kuzalishwa kwa ajira hizo, vikundi 709 vimeanzishwa na wanufaika 15,124 wamefanikiwa kujikwamua kutoka katika umaskini. Alibainisha kuwa maono ya Hand in Hand Eastern Africa ni kuona jamii inayowezeshwa kiuchumi kupitia biashara na ajira endelevu, huku dhamira yake ikiwa ni kuwawezesha wanawake na jamii zao kujiondoa katika umaskini.
Alisema shirika hilo limekuwa likitekeleza shughuli zake kwa kuanzisha vikundi vinavyowawezesha wanawake na wanaume kujifunza pamoja, kuweka akiba na kuimarisha uwezo wao wa kiuchumi. Pia limekuwa likitoa mafunzo ya biashara na ujasiriamali yanayojenga ujuzi, kujiamini na uwezo wa kuendesha biashara kwa ufanisi.
Aidha, Temu alisema shirika hilo limekuwa likiwaunganisha wanachama wake na taasisi za kifedha pamoja na watoa huduma za mikopo ili kuwawezesha kupata mitaji na kukuza biashara zao.
Kwa upande wake, Meneja wa Miradi ya Mnyororo wa Thamani wa shirika hilo, Lucas Michael, alisema wafugaji wa kuku 3,120 wamepatiwa mafunzo kuhusu mbinu bora za ufugaji wa kuku, lishe, afya ya mifugo, usimamizi wa biashara pamoja na utunzaji wa kumbukumbu za kifedha na uzalishaji.
Alisema mafunzo hayo yamechangia kuongeza tija katika ufugaji wa kuku na kuwawezesha wafugaji kupata bidhaa zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.
Kwa upande wake Meneja Jumuishi wa Fedha kutoka Hand in Hand Eastern Africa Tanzania, Amos Isaya,alisema shirika limeandaa Jukwaa la Uunganishaji wa Masoko (Market Linkage Forum) kwa wadau wa sekta ya ufugaji wa kuku, likiwa na lengo la kuwajengea wanufaika wake fursa za masoko na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya wazalishaji na wanunuzi wa mazao ya kuku.
Jukwaa hilo linawaleta pamoja wafugaji wa kuku wanaonufaika na miradi ya shirika hilo, wanunuzi wakubwa, wasindikaji wa bidhaa za kuku, taasisi za kifedha pamoja na wadau wengine wa maendeleo ili kujadili namna bora ya kukuza biashara na kuongeza tija katika sekta hiyo.
Isaya alisema kuwa lengo kuu ni kujenga soko lenye fursa na mahusiano madhubuti ya kibiashara yatakayowawezesha wafugaji kupata masoko ya uhakika kwa bidhaa zao.
Alisema kuwa kwa kuwaunganisha wazalishaji na wanunuzi, shirika hilo linaamini litasaidia kuongeza upatikanaji wa masoko yenye tija, kukuza mauzo na kuwawezesha wanufaika wake kupanua biashara zao kwa ufanisi zaidi.
“Tunatambua kuwa changamoto ya masoko ni moja ya vikwazo vikubwa kwa wafugaji wengi wa kuku. Kupitia jukwaa hili, tunalenga kujenga mazingira yatakayowawezesha wazalishaji kuingia katika mikataba ya kibiashara na wanunuzi mbalimbali kwa manufaa ya pande zote,” ilieleza sehemu ya taarifa ya waandaaji.
Mbali na kuunganisha masoko, jukwaa hilo pia litatoa fursa kwa washiriki kukutana na kubadilishana uzoefu, maarifa na mbinu bora za ufugaji wa kisasa, huku wakichunguza fursa za ushirikiano zitakazosaidia kukuza sekta ya ufugaji wa kuku nchini.
MWISHO






Post a Comment