Na Sylvester Richard.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida limewakamata na kuwafikisha mahakamani Chacha Marwa Sandu (24) na Michael Steven (48) wakazi wa Bugugu relini mkoani Mwanza kwa tuhuma za mauaji ya walinzi wawili waliouwawa katika maeneo na nyakati tofauti.
Akiongea na Waandishi wa Habari ofisini kwake, Juni 19, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Amon D. Kakwale amesema kuwa, mauaji hayo yalitokea Aprili 19, 2024 katika Manispaa ya Singida, Kata ya Misuna ambapo watuhumiwa walimuua Elvis Muna (65) aliyekuwa akilinda duka na kufanikiwa kuiba vitu mbalimbali ikiwemo simu 2 ndogo za Tecno na smartphone 2 aina ya Infinix na Sumsung.
Aidha, Kakwale amesema, siku hiyohiyo watuhumiwa hao wakiwania mali, walimuua Ismail Ramadhan (37), mlinzi wa kampuni ya ulinzi ya 'New Imara' aliyekuwa akilinda grosari ijulikanayo kwa jina la 'Supa kitasa' ambapo walijaribu kuvunja mlango wa grosari kwa lengo la kuiba. Baada ya kutekeleza mauaji hayo, walitokomea kusikojulikana.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Singida lilifanya msako kuwatafuta watuhumiwa kwa kushirikiana na raia wema na kufanikiwa kuwakamata Mei 26, 2024 huko Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga ambapo walisafirishwa hadi Singida na kuwafikisha mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.
Kutokana na ukamataji huo, Jeshi la Polisi linawashukuru wananchi wote waliosaidia kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kuendelea kuwasisitiza waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu wengine ili nao wakamatwe kwa njia iliyo salama na kufikishwa mahakamani, jambo ambalo litaimarisha usalama wa Mkoa wa Singida.
No comments: