Na Amini Nyaungo
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari Samia Suluhu Hassan anaelekea kufikisha miaka mitano mwakani katika uongozi wake amefanya mengi na makuu sana ambayo kama nchi waliowengi wanampongeza kwa kazi nzuri anayoifanya, japo katika shilingi kuna pande mbili wapo wa wanaopongeza na wapo ambao hawaoni kinachofanyika. Hii ipo kila nchi na falsafa ya maisha inasema ukipendwa na jamii yote basi wewe sio binadamu inatakiwa ujitafakari sana kawaida inatakiwa uwe na pande mbili hivyo hii ni dalili ya kuwa Samia amefanikiwa ana maaduii na ana watu wema. Kwa yale aliyoyafanya sisi Chamber Media tunampongeza na tumeamua kupanga kikosi chake cha mashambulizi mithili ya mpira na tukitaja sifa za kila aliyepata namba katika kikosi chake. Na hapa tunaangalia waliopo serikalini hadi wale waliopo katika chama hata vyama vingine kama wamekidhi vigezo vya kuingia katika "Lineup" kikosi chake.
Katika kikosi hiki yeye anabakia kuwa kocha mkuu mwenye leseni ya ukocha FIFA Leseni A.
1. Dokta Philip Isdori Mpango
Huyu ni Makam wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kabla ya hapo alikuwa Waziri wa Fedha lakini mara tu baada ya Samia kuingia madarakani aliona Mpango anamfaa kumsaidia kazi. Ni kweli Mpango ni mchapakazi pamoja na anayejali sana utu wa mtu huku akiwa na hofu ya Mungu sasa hapa wamekutana Samia anahofu ya Mungu na yeye basi hiyo Kombinasheni yake mie hata sitaki kusema neno. Mpango ana vigezo vyote vya kuingia katika kikosi hiki anastahili na hana mbadala yaani "Substituion" kazi yake inaonekana wala haihitaji kuhadithiwa sana kwa hakika hii ilikuwa chaguo zuri sana kwa Samia kuweza kumsaidia kazi.
2. Kassim Majaliwa
Majaliwa anatudhirishia kuwa kuna muda uongozi wala hauhitaji PHD wala Profesa bali Mungu humpa amtakaye kariba ya uongozi. Ukiniambia mie baada ya Samia 2030 kupitia chama chao cha Mapinduzi CCM nani atafaa kuwa Rais nakwambia Majaliwa ana sifa zote za kuwa katika Mamlaka anajua sana ana hekima sana pamoja na utekelezaji.
Majaliwa ameweza kuyafanya mengi akiwa Waziri Mkuu wakati wengi hawakutarajia nani atakuwa Waziri Mkuu Rais aliyepita Magufuli aliuonesha Umma wa Watanzania kuwa kuna mtu kutoka Luangwa Lindi anaweza kuwa kiongozi mkubwa na akafanya makuu hivyo alianza kupata namba akiwa kwa Magufuli hadi Samia namba bado anayo na anatamba nayo. Naamini kama 2025 mambo yakiwa sawa na wakirudi wote basi itakuwa kazi rahisi kwake kupata nafasi ya namba na hivi ameweka wazi kuwa atagombea Ubunge katika jimbo lake ni ishara ya kuwa anarudi na kama mama akirudi basi na yeye atasalia katika nafasi yake. Hebu tukumbuke yale maandamano ya wafanyabiashara pale Kariakoo wakati ule akiyasawazisha na watu kurudi katika hali ya kawaida pamoja na sehemu nyingine akiwaondoa wale wabadhilifu.
Kassim Majaliwa mitano tena anaweza na anatosha hivyo katika kikosi hiki yeye beki namba mbili akiwakaba wale wote wasumbufu.
3. Dokta Doto Biteko
Kuna muda Wasukuma wanakariba ya uongozi hivi na wanafanyakazi kweli au ndio ile kauli inayosema mzigo mzito mpe Msukuma ? Huenda ikawa kweli. Biteko yeye ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati anafanya vizuri sana kwake yeye vitendo vingi kuliko maneno na ndio viongozi tunaowataka.
Sina mashaka naye katika utendaji wa kazi Tanesco juzi hapo tu waemachana na Songas na kujitegemea baada ya kujitosheleza,lakini zile vurugu za nyuma za umeme hazipo sasa hivi hivyo anatosha sana. Wengi wanajiuliza kuwa kwanini awe Naibu Waziri Mkuu ? Kwani Majaliwa peke yake hatoshi ? Wengine wakienda mbali zaidi wakisema kuwa uwepo wake kama Naibu Waziri Mkuu ni taa ya kijani kwa Majaliwa.
Shida ya wabongo wape picha tu kishaa waachie wao maelezo watamaliza wenyewe ndio ilivyo tunadanganyana sana huko mtaani lakini ukweli ni kwamba hii nafasi ya Naibu Waziri Mkuu 1995 alifanyika kwa Mrema lakini hata kama haikuwepo shida iko wapi? Sio kila kitu kiwe na maelezo ni jambo zuri sana kazi ya Naibu kama Waziri hayupo yeye anashika nafasi yake na kazi inaendelea, mbona waziri wa Madini ana msaidizi wake kwanini hii kila mtu ananyanyua panga ?
Biteko anafanyakazi nzuri na anaingia moja kwa moja katika kikosi cha Samia kwa uwezo wake wa kufanya kazi , hiki kikosi huingii hivi hivi lazima uwe mchapakazi.
Doto ana kaka yake Kulwa yeye hakupata nafasi ila nashauri hata huyu kaka yake anafaa kwa namna tunavyomuona Doto.
4. Paul Makonda
Uthubutu, Upekee pamoja na kupenda kuwa mbunifu ndio sababu ya Makonda kuingia katika kikosi akipewa jezi namba nne akizuia na kutoa mashambulizi. Makonda anajua sana kazi anajua sana kukaa katika eneo lake ili asishambuliwe na adui, huyu anatakiwa atembee mikoa yote Tanzania ili ubunifu na uthubutu alionao ufanyekazi na mikoa ipate maendeleo anafanya vyema sana anafanya vitu bila kuogopa japo kwa jicho la kawaida lazima uwe muoga kuweza kuyafanya ila yeye anayafanya.
Makonda tangu ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha amefanya vitu vingi sana vizuri ikiwemo ubunifu kwa ajili ya kuwaleta watalii katika siku ya Rang Rover na Land Rover pamoja na usaidizi wake anapokuwa katika vikao mbalimbali. Naamini utendaji kazi wake ndio unamfanya kila siku azidi kung'ara anafanyakazi nzuri na kila mmoja anaona kila kitu anachofanya.
Wakati Rais Samia akimtoa katika Chama na kumpeleka kuwa Mkuu wa mkoa wa Arusha wengi wamelia sana lakini Samia alijua huku atasaidia zaidi na ndio maana alimpa nafasi hiyo na kweli ukiwauliza "Wadudu" pale Chuga kuwa Makonda ahamishwe watakukimbiza na panga wakitaka abakie na aendelee kufanyakazi vizuri katika mkoa wao .
Chamber Media tunakutakia kila la kheri Makonda na katika hiki kikosi upo na unepewa namba nne ya bahati.
5. Juma Aweso
Mtoto kutoka familia za kawaida kabisa kama ambayo nilivyo mimi mwandishi Mungu anampa talanta ya uongozi na anakuja kufanya makuu , Juma Aweso ni mmoja tu hapa nchini kwanini ? Aweso ni Waziri wa Maji kitengo kigumu mno tena yeye amedumu kweli kweli vinginevyo angekaa benchi hivi sasa anapiga kazi usiku na mchana ili maji yapatikane kila sehemu kazi yake ni kubwa mno , nafahamu kuna sehemu nyingine maji hayajafika ila kupitia yeye kadri siku zinavyoenda mambo yatakuwa sawa na Watanzania watafurahia uwepo wake katika Wizara hiyo.
Kitu pekee kwa sasa kinachompa doa kuwepo kwa mgao wa maji karibuni mikoa mingi hapa Tanzania jana nilikuwa Dodoma nimekuta mgao huku Singida kadhalika, lakini hii haitunyimi kumpa namba katika kikosi cha Samia anajituma anaiwezea sana Wizara hii ya Maji na tuendelee kumwambia kuwa kazi iendelee ukija kwa Wanyaturu wanakwambia "Wajefya sana" maana yake Ahsante sana. Aweso anakaaa na Makonda wazuie maadui nikisema wazuie maadui simaanishi watu bali kufanya vyema katika sekta zao ili taifa liende vyema.
6.Jerry Silaa
Huyu ni Waziri wa Habari lakini namba kaipatia akiwa Waziri wa Ardhi huku ndio mambo yake makubwa yalionekana, hakuwa muoga kuamua jambo lakini sio kuamua bali anaamua kwa kufuata utaratibu na kanuni aliiwezea sana ile Wizara. Ile sera yake ya maeneo ya watu na kuwepo kwa sheli, Silaa alifanya Taikuni wote mjini walimchukia kwa maamuzi yake hii ilifanya kila mtu akumbuke uwezo wake akiwa katika Wizara ya ardhi. Huku katika habari bado mimi sijaona cheche zake lakini bado nina imani atafanya vizuri, nasema hivyo kwakuwa nafahamu uwezo wake pamoja pia kufahamu Wizara ya habari pamoja na vyombo vya habari madudu yake.
Silaa anakula kiungo mkabaji katika kikosi cha Samia unasemaje ? Naamini anafaaa kuingia katika kikosi.
7. William Lukuvi
Wakati anatolewa Wizara ya Ardhi kila mmoja alitaka kulia kwa kazi nzuri aliyoifanya lakini Rais alitaka busara zake Ikulu sio kazi rahisi kuwa mshauri wa Rais, unajua pale kwake Rais kuna mambo mengi sana mara mikataba mara mahusiano na nchi na mengineyo hivyo alihitaji watu wazoefu na ikumbukwe ndio aliingia madarakani kwangu mimi ilikuwa jambo jema sana. Kazi yake imetukuka sasa amerudi na amechukua kitengo Lukuvi anakula shavu la kushoto winga teleza akamimine maji watu wafunge. 8. Prefesa Adolf Mkenda
Huyu tunampa dimba atawale kutokana na umuhimu wa elimu katika taifa, lakini sio tu anapata namba bali anafanyakazi inayotakiwa katika Wizara ya Elimu kwanini asipate namba katika kikosi hiki ? Unadhani kwanini tumempa namba, mimi pia ni mmoja ya watu wanaoona elimu yetu inamzunguko sana sasa yeye alivyoingia kaleta mabadiliko sasa tutaenda hadi darasa la sita na baada ya hapo Kidato cha kwanza japo bado elimu ni ndefu mno anatakiwa afanye makeke ipungue zaidi.
Uwepo wake harakati zake zinatufanya tuzidi kuamini kuwa dimba namba nane analiweza na anaweza kuunganisha timu ya Samia kufika kileleni mwa msimamo wa ligi. 9. Dokta Tulia Akson
Huyu mama hana haja ya kumuelezea ni mtu ambaye anafanya vyema katika uongozi alivyoanza kama masikhara lakini kumbe ni "Mnyama"sana katika kazi , nikimaanisha anafanya vizuri unyama maana yake anafanya vyema. Uwezo wake wa kutafasiri sheria na kujiamini sio tu katika Bunge la Tanzania bali hata nje kumbuka yeye ndio Rais wa Mabunge duniani IPU ana misimamo inayofuata sheria na siasa zisizo na chuki. Mbunge wa Mbeya mjini, tumempa nafasi ya kuwa mshambuliaji kutokana na jukumu lake zito kuanzia hapa kwetu katika Bunge hadi huko duniani, anafaaa sana na hapa hakuna atakaye uliza kwani amepewa jukumu zito la kuunganisha timu kutoa furaha huyu Tulia anafaaa.
Licha ya mambo ya Kibunge anatoa faraja katika Taasisi yake ya Tulia Trust wengi wamefanikiwa lakini pia ukiingia katika page yake ya Instagram huwa anatoa faraja kwa wafuasi wake kwa kuwatumia chochote kitu akijua kuwa maisha hayafanani. Huyu ndio mfungaji wetu, na urefu wake na mwili anaweza akatusaidia tupate magoli mengi.
Kitu pekee ambacho hujui hii ndio silaha moja wapo ya Samia kuelekea katika nchi ya ahadi. 10. Queen Cathbert Sendiga
Huyu alionwa na Magufuli alikiwa chama cha ADC amepata namba alisema sitokosea nafanyakazi kwa bidii, ukitaka ugombane na Samia mwambie Sendiga hafai hahahaha , Sendiga hahitaji sana maelezo, huyu ana ubunifu na uthubutu katika majukumu yake. Hakuna Rais asiyetaka huduma yake anafanyakazi nzuri Manyara kwa Jeografia yake ni ngumu kuiongoza lakini yeye anafanya mambo yanaonekana kuwa rahisi kwa kazi nzuri anayoifanya , anastahili pongezi sana. 11. Dokta Emanuel Nchimbi
Huyu sasa anatokea ndani ya Chama cha cha Mapinduzi , uwezo wake wa kujenga hoja na kutaka siasa za Demokrasia ndio imenifanya nimuweke katika kikosi hiki, Nchimbi hatakk siasa za malumbano weka mpira kati tuchakate kwa hoja. Hii itamfanya hata viongozi wenzake ndani ya chama wamchukiekwa misimamo yake, ni mtu ambaye anayejua sana Diplomasia anaweza sana kumjenga mtu anaingia katika kikosi hiki moja kwa moja wala hana mpinzani na anasaidia sana kuweza kuunganisha kati ya serikali na chama, kifupi tumemuweka namba 11 amwage maji streka lifunge goli.
Nchimbi atamfikisha nchi ya ahadi Samia kwa namna anavyoendesha siasa zake namna ya kuweza kuwakabili wapinzani zile 4R za Samia anaziishi kabisa. Nchimbi ana utu ndani yake, mimi niliwahi kumuomba msaada flan hivi zamani sana miaka 14 iliyopita hanijui hajaniona ila alinisaidia.
Kuna mtu ana swali katika kikisi hiki ? Sema nani atoke aingie nani ?
Mwisho kabisa niweke wazi tu kuwa Samia tunatamba naye na tunaishi naye kwa yote mazuri ambayo anayafanya kutengeneza shule za msingi na sekondari, miradi mikubwa ya maendeleo unadhani kazi rahisi ingie wewe uone inavyokuwa ngumu.
Mwisho
No comments: