Wakuu wa Shule 12,000 Kunufaika na Mafunzo ya Uongozi Kuimarisha Elimu Nchini

 

Na Mwandishi Wetu, Mwanza



SERIKALI imezindua rasmi mafunzo ya uongozi kwa wakuu wa shule za sekondari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar katika hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa elimu na kuongeza ubora wa utoaji wa huduma za elimu nchini.


Mafunzo hayo yamezinduliwa Mei 28, 2026 jijini Mwanza na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, ambaye amesema viongozi wa shule wanapaswa kupewa uwezo wa kutosha ili kusimamia taasisi zao kwa ufanisi, uwajibikaji na weledi unaoendana na mahitaji ya sasa ya sekta ya elimu.



Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Prof. Nombo alisema mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha mifumo ya uongozi wa shule, kuongeza uwajibikaji kwa viongozi wa elimu pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora inayokidhi viwango vinavyotarajiwa.



“Ni muhimu kwa viongozi wa shule kuwa na uwezo wa kusimamia taasisi zao kwa ufanisi, uwajibikaji na maadili ya kitaaluma ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu yenye ubora unaotarajiwa,” alisema Prof. Nombo.


Aidha, aliipongeza Taasisi ya ADEM kwa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mafunzo hayo yanayotolewa kupitia ushirikiano kati ya taasisi hiyo na mradi wa LiT-LEAD Tanzania, akisema ushirikiano huo unaendelea kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya elimu nchini.



Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, alisema mafunzo hayo yana umuhimu mkubwa kwa wakuu wa shule za sekondari nchini kutokana na ukweli kuwa kwa muda mrefu viongozi hao hawajapata mafunzo ya kina ya kiuongozi na kiutendaji.


Alisema kupitia mafunzo hayo, wakuu wa shule watapata maarifa na mbinu mpya zitakazowawezesha kusimamia shule kwa ufanisi zaidi, kujenga mazingira bora ya kujifunzia pamoja na kuongeza ufaulu wa wanafunzi.


“Mafunzo haya yatawasaidia viongozi wa shule kwenda sambamba na mabadiliko ya sekta ya elimu na kuongeza uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika usimamizi wa shule,” alisema Dkt. Maulid.


Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI, wathibiti ubora wa shule, maafisa elimu wa mikoa na wilaya pamoja na wadau wa elimu kutoka maeneo mbalimbali nchini.



Mradi wa LiT-LEAD Tanzania unatarajiwa kutoa mafunzo kwa wakuu wa shule za sekondari 12,000 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, huku ukilenga kuwafikia zaidi ya wanafunzi milioni 2.8 kupitia maboresho ya uongozi na usimamizi wa shule.


MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post