TAKUKURU MKOA WA SINGIDA YAWAPANDISHA KIZIMBANI WATATU AKIWEMO ALIYEKUWA MGANGA MFAWIDHI HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SINGIDA

 Na Jumbe Ismailly SINGIDA



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Singida imewapandisha kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida watu watatu akiwemo aliyekuwa Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida,Deogratias Gosbert Banuba kwa tuhuma za kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri na matumizi mabaya ya mamlaka na kuisababishia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida hasara ya shilingi 75,130,328/=

Mawakili wa serikali Dorothea Kinyonto na Yvonne Munisi walidai kuwa kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 14691/ 2026 iliyofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida inawahusisha aliyekuwa Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida,Deogratias Gosbert Banuba,Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida,Emmanuel Osward Matola na Erick Richard Mtega Mfanyabiashara kwa jina la PLUSTECH LIMITED.

Aidha Mawakili hao walida pia kwamba washtakiwa hao walitenda makosa hayo kati ya tarehe 01/12/2020 na30/ 07/2021,hivyo wanakabiliwa na tuhuma za makosa ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri kinyume na kifungu cha 22,matumizi mabaya ya mamlaka kinyume na kifungu cha 31 vifungu vyote hivyo chini ya sheria ya kuzuia na Kupambana na Rushwa sura ya 329 marejeo ya 2019 ikisomwa pamoja na aya ya 21 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1)na 60(2) vyote vya sheria ya Kudhibiti uhujumu uchumi na makosa ya kupangwa sura ya 200 marejeo ya 2019.

Kwa mujibu wa Mawakili hao washitakiwa hao waliisababishia mamlaka hasara kinyume na aya ya 10(1) ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vyote vya sheria ya Kudhibiti uhujumu uchumi na makosa ya kupangwa sura ya 200 marejeo ya 2019 na utakatishaji fedha kinyume na kifungu cha 12(d) na ( e ) vya sheria ya kudhidbiti utakatishaji fedha sura ya 423 marejeo ya 2019 ikisomwa pamoja na aya ya 22 ya jedwali la kwanza na vifungu vya 57(1) na 60(2) vyote vya sheria ya kudhibiti uhujumu uchumi na makosa ya kupangwa sura ya 200 marejeo ya 2019.

Katika kesi hiyo inayosikilizwa na Mheshimiwa Hakimu Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida, Allu Nzowa,Mawakili,Dorothea na Yvonne walidai kwamba Emmanuel Osward Matola alisaini nyaraka ambazo ni hati za uwasilishaji vifaa kwa lengo la kuonesha kwamba mzabuni PLUSTECH LIMITED amewasilisha vifaa vinavyoonekana kwenye hati hizo huku akijua kwamba mzabuni huyo hakuwasilisha vifaa vyenye thamani ya shilingi 73,130,328/=.

Mshitakiwa Erick Richard Mtega aliwasilisha hati za uwasilishaji vifaa kwa lengo la kuonesha kwamba Kampuni ya PLUSTECH LIMITEG imewasilisha vifaa vyote vinavyoonekana kwenye hati hizo huku akijua kwamba vifaa vyenye thamani ya shilingi 73,130,328/= havikuwasilishwa na hivyo kujipatia manufaa yasiyostahili.

Kwa mujibu wa Mawakili hao mshitakiwa Deogratias Gosbert Banuba akiwa Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida,alitumia mamlaka yake vibaya kwa kuidhinisha hati za malipo zilizomlipa mzabuni PLUSTECH LIMITED bila kujihakikishia usahihi wa nyaraka zote za mchakato wa malipo,hivyo kwenda kinyume na Kanuni ya Fedha za umma za mwaka 2001 na kupelekea mzabuni huyo kupata manufaa yasiyostahili ya shilingi 73,130,328/=.

Walidai wanasheria hao kwamba washitakiwa wote kwa pamoja wanakabiliwa na tuhuma za kosa la kuisababishia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida hasara ya shilingi 73,130,328/= kutokana na uzembe wao wakutotekeleza majukumu yao ipasavyo.

“Pia washitakiwa wote wanakabiliwa na tuhuma za kosa la utakatishaji fedha ambapo mzabuni aliweza kujipatia kiasi cha shilingi 73,130,328/= na washitakiwa wengine wakimuwezesha mzabuni kutenda kosa hili huku wakijua au walipaswa kujuwa kwamba wakati wakimsaidia mzabuni na wakati mzabuni akipokea fedha hiyo,ilikuwa ni zao la uhalifu kutokana na makosa tangulizi ambayo ni kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri na matumizi mabaya ya mamlaka”walisisitiza Mawakili hao.

Washitakiwa wote wako mahabusu kwa kukosa dhamana kutokana na kukabiliwa na kosa la utakatishaji fedha ambalo halina dhamana hadi julai,08.mwaka huu kwa ajili ya kusoma hoja za awali.

MWISHO.


Post a Comment

Previous Post Next Post