TUZO YA WSIS NI MATUNDA YA UONGOZI WA DKT. SAMIA - WAZIRI KAIRUKI

 

Na Prosper Makene 

 


Geneva, Uswisi, Julai 09, 2026– Tanzania imepata heshima ya kutunukiwa Tuzo ya Kimataifa ya WSIS Prizes 2026 kutokana na mafanikio ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano. Mradi huo umeongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na ambayo awali hayakuwa na huduma ya mawasiliano nchini.


Tuzo hiyo imepokelewa na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb.) katika hafla iliyofanyika Geneva, Uswisi. 


Akizungumza mara baada ya kuipokea tuzo hiyo, Waziri Kairuki amesema tuzo hiyo ni matunda ya uongozi thabiti wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano nchini.


“Rais Samia amedhamiria kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya mawasiliano bila kujali alipo. Tuzo hii inathibitisha kuwa juhudi zetu za kufunga pengo la kidijitali zinatambuliwa kimataifa,” alisema Waziri Kairuki.


Mradi wa ujenzi wa minara 758 ulizinduliwa rasmi na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 10 Aprili, 2026.



Mbali na kutwaa tuzo hiyo, Tanzania ilipata uteuzi katika vipengele saba (7) vya Tuzo za WSIS 2026 na kufanikiwa kuibuka na tuzo mbili kwa ujumla. Nchi pia imetunukiwa vyeti vya kutambua miradi mingine iliyofanya vizuri.


Tuzo za WSIS hutolewa kila mwaka na Umoja wa Kimataifa wa Mawasiliano ITU kutambua miradi bora inayochangia katika kufikia malengo ya Mkutano wa Dunia kuhusu Jumuiya ya Habari.


Mwisho

Post a Comment

Previous Post Next Post