Na Jumbe Ismailly MANYONI May,20,2026 Malisho
WIZARA ya Maliasili na Utalii imeombwa kuangalia uwezekano wa kusogeza mipaka yake kwenye vijiji vinavyopakana na maeneo ya mapori yake ya Akiba ili mifugo ya wafugaji waliopo katika vijiji vinavyozunguka hifadhi hizo iweze kupata malisho ya kutosha.
Wafugaji wa Kata ya Mitundu,Halmasghauri ya Itigi, wilayani Manyoni walipaza sauti ya ombi hilo kwenye mkutano wa hadhara wa kusikiliza kero za wafugaji na Mbunge wa jimbo la Itigi,wilayani Manyoni,Mkoani Singida.
Akiwasilisha kero hiyo kwa mbunge wa jimbo hilo, Kiongozi wa wafugaji hao,Omari Bakari Makanja,maarufu kwa jina la Mwananyiinzi aliweka bayana kwamba wafugaji wa Kipera au watu kata ya Mitundu kwa ujumla wana kilio cha malisho ya mifugo yao.
“Kilio chetu watu wa Kipera au kata ya Mitundu kwa ujumla,tuna kilio cha machungio tunahangaika sana tunahangaika sana ng’ombe zetu mpaka tumepeleka Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Mbeya,tunaomba machungio utupe machungio.
Kiongozi huyo wa wafugaji alisisitiza kuwa ili waweze kuondokana na kero ya upatikanaji wa malisho ya mifugo yao,wanaiomba serikali kupitia wizara ya maliasili isogeze mipaka ya mapori yake kutoka kwenye baadhi ya vijiji vinavyozunguka ili wafugaji wake waweze kupata malisho ya kutosha ikilinganishwa na hali iliyopo kwa sasa.
“Kuhusu huku kupanuliwa kwa maeneo ya game reserve kwani kulikuwa na eneo la wazi,lakini kwa sasa eneo hilo limewekewa kizuizi ambacho kimewabana wafugaji na hadi kukosa mwelekeo,hivyo tunaomba utusaidie kuanzia maeneo ya Uswesa hadi maeneo ya Makunguni”alisisitiza Bakari.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Manyoni,Jumanne Ismaili Makhanda akizungumza katika mkutano huo alikiri kwamba changamoto zilizotolewa na wafugaji wa kata hiyo wao kama chama wameyachukua na hata kuyaona kwa macho pia.
Mwenyekiti Makhanda alibainisha kuwa kupitia kero za wafugaji hao ni kwamba maeneo ya malisho ya mifugo hayatoshelezi mahitaji ya mifugo yao na hivyo kuiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuyarejesha maeneo waliyomega ili wapate maeneo ya kuchukungia.
“Lakini ombi lao ni kutaka eneo lililopo la hifadhi au eneo ambalo lilikuwepo zamani kwenye Kijiji baadaye likasogezwa wakaweka bikoni kama sikosei mlisema hivyo,wanaomba eneo lao lililosogezwa lirejeshwe ili kusudi waweze kupata mahali pa kuchungia na mmeleta sauti hiyo sehemu sahihi kwa mbunge na kwa chama cha mapinduzi na kwa daktari Samia Suluhu Hassani” alifafanua Makhanda.
Alifafanua Makhanda kwamba kwa sababu Daktari Samia Suluhu Hassani na serikali yake yuko kwa ajili ya wananchi,yuko kwa ajili ya kusikiliza watu,yuko lakini kwa ajili ya kuwatumikia watu na anafanyakazi usiku na mchana.
Akizungumzia ombi la wafugaji juu ya kusogezwa kwa mpaka,Mbunge wa jimbo la Itigi,Yohana Stephen Msita alisema kwamba anajua serikali ina mpango wa muda mrefu wa kuweka uzio,lakini hata hivyo alitumia wasaa huo kuuomba uongozi wa pori la akiba kwamba mara wananchi wanapotoa taarifa ya tembo kuingia kwenye maeneo ya makazi,askari wa wanyamapori wawe wakifika kwa wakati.
“Jingine wako wananchi hawa umekisikia mifugo ni mingi sana ikitokea wameingia kwa bahati mbaya lakini hawajaingia sana mkakamata mifugo mnaongea nao kwa upendo siyo mpaka muwapige,muwanyang’anye mifugo, muwatoze mafaini hawa ndiyo wamekuwa wakilinda haya mapori miaka nenda rudi kabla hata nyie hamjayaona.
Kamanda wa Uhifadhi,Pori la Akiba Muhesi,Paul Lunimba alisema hoja ya wafugaji wa Kijiji cha Ipalalyu ameipokea na ataifikisha sehemu panapohusika na mrejesho wake ataurejesha kwa Mbunge huyo ili wananchi wajue kinachoendelea.
Post a Comment