Na Sophia Daniely – SINGIDA
Utaratibu wa Parole umeendelea kuleta mabadiliko chanya kwa wafungwa waliorekebishwa tabia zao, ambapo Bw. Emmanueli Matoke, anayetumikia kifungo chake akiwa uraiani, ameanza kujitegemea kiuchumi kupitia ujuzi alioupata akiwa gerezani.
Bw. Emmanueli aliachiliwa kwa utaratibu wa Parole baada ya kutumikia kifungo chake kwa kipindi cha miaka miwili na nusu. Akiwa gerezani, alipata mafunzo ya ujenzi kupitia programu za urekebishaji zinazoratibiwa na Jeshi la Magereza.
Akizungumza katika eneo lake la kazi, Bw. Emmanueli amesema kuwa mafunzo aliyoyapata gerezani yamekuwa chachu ya mabadiliko ya maisha yake, akieleza kuwa “Parole imenipa nafasi ya pili ya kuishi kwa heshima na kuendelea kuitumikia familia yangu pamoja na jamii,” alisema Bw. Emmanueli.
Kupitia kazi zake za ujenzi, Bw. Emmanueli amekuwa akitoa huduma kwa wananchi wa maeneo mbalimbali katika Mkoa wa Singida, huku akiwahamasisha vijana kujiepusha na vitendo vya kihalifu.
Hatua hiyo inaonesha kuwa utaratibu wa Parole ni nyenzo muhimu ya urekebishaji inayowawezesha wafungwa kubadilika na kuwa raia wema na wenye mchango katika maendeleo ya taifa.
Mwisho





Post a Comment