MAAFISA 90 WA JESHI LA MAGEREZA WAHITIMU SHAHADA YA UZAMILI CHUO CHA UHASIBU ARUSHA

 

Na SGT Sophia Daniely – ARUSHA



Naibu Waziri wa Fedha, Mheshimiwa Laurent Lusetula (Mbunge), amewatunuku shahada ya uzamili wahitimu 2,250 wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), wakiwemo maafisa na askari 90 wa Jeshi la Magereza, waliosajiliwa katika mwaka wa masomo 2024/2025 katika fani mbalimbali zikiwemo amani na usalama pamoja na uongozi na utawala. Mahafali hayo yamefanyika Februari 06, 2026, katika ukumbi wa Ngurudoto jijini Arusha.




Akizungumza katika mahafali hayo, Mheshimiwa Lusetula amewataka wahitimu wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kutumia elimu waliyoipata kama chachu ya kuleta maendeleo ya taifa.



“Nendeni mkaitumie vyema elimu na maarifa mliyoyapata ili kuchochea maendeleo ya taifa. Zingatieni misingi ya amani na muwe wazalendo,” alisema Mheshimiwa Lusetula.



Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha, Profesa Eliamani Sedoyeka, alimshukuru Mkuu wa Jeshi la Magereza kwa ushirikiano wa dhati uliopo kati ya chuo hicho na Jeshi la Magereza kupitia programu mbalimbali zinazowawezesha maafisa na askari kupata elimu itakayowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao, hususan katika shughuli za urekebishaji wa wafungwa na mahabusu.




Aidha, Mrakibu wa Jeshi la Magereza (SP) Amos Atanas Maheri, ambaye ni miongoni mwa wahitimu wa shahada ya uzamili katika Chuo cha Uhasibu Arusha, ametunukiwa zawadi maalum baada ya kufanya vizuri zaidi katika masomo ya uongozi na  utawala.

Post a Comment

Previous Post Next Post