Na Mwandishi Wetu
VIJANA wenye ulemavu mkoani Singida wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali, hususan mikopo ya asilimia 10 inayotengwa na halmashauri kwa ajili ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, ili kujiinua kiuchumi na kuboresha maisha yao.
Wito huo umetolewa na Afisa Maendeleo ya Vijana wa Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani, wakati wa ziara yake ya kukagua na kufuatilia shughuli za vikundi vya vijana katika maeneo yao ya utekelezaji wa miradi ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, mkoani Singida.
Ndahani alisema Serikali imeweka mazingira rafiki na sera zinazolenga kuhakikisha kundi la watu wenye ulemavu haliachwi nyuma katika mchakato wa maendeleo, huku akisisitiza kuwa fursa hizo zipo wazi kwa wote wanaokidhi vigezo na wenye nia ya dhati ya kufanya kazi.
“Serikali imedhamiria kuwawezesha vijana wote bila ubaguzi. Vijana wenye ulemavu hawapaswi kuona ulemavu wao kama kikwazo, bali kama changamoto ya kugeuza fursa zilizopo kuwa chanzo cha maendeleo na ajira,” alisema Ndahani.
Aliongeza kuwa mikopo hiyo inalenga kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendeleza shughuli za uzalishaji mali ikiwemo kilimo, ufugaji, biashara ndogondogo pamoja na huduma mbalimbali, hatua itakayosaidia kupunguza utegemezi na kuongeza kipato cha kaya.
Afisa huyo wa vijana aliwasisitiza wanufaika wa mikopo hiyo kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, kusimamia miradi yao kwa uadilifu na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati ili kutoa fursa kwa vijana wengine wengi zaidi kunufaika.
Ndahani aliwahakikishia vijana hao kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na halmashauri itaendelea kutoa ushauri, ufuatiliaji na mafunzo ili kuhakikisha miradi yao inakuwa endelevu na yenye mafanikio kwa muda mrefu.
Naye Afisa Maendeleo ya Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Peterson Ngahava, alisisitiza umuhimu wa vijana kurejesha mikopo yao kwa wakati na kwa hiari, akieleza kuwa nidhamu ya urejeshaji hujenga uaminifu kati ya vijana na Serikali na kuwezesha vijana wengine wengi zaidi kunufaika na mikopo hiyo.
Kwa upande wao, baadhi ya vijana wenye ulemavu walionufaika na mikopo hiyo wilayani Iramba walishukuru Serikali kwa kuwawezesha, wakieleza kuwa mikopo hiyo imewapa matumaini mapya ya kujitegemea kiuchumi na kujiona sehemu ya jamii inayochangia maendeleo.
Walisema kupitia mikopo hiyo, wamefanikiwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi ambayo imeanza kuwaletea kipato, huku wakiomba kuendelea kupewa elimu ya ujasiriamali na usimamizi wa miradi ili kuongeza tija.
Mmoja wa wanufaika kijana mwenye ulemavu wa ngozi, Abdallah Shalua, aliyenufaika na mkopo wa Serikali wa shilingi milioni saba (7,000,000) kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza duka la bidhaa mchanganyiko, hatua iliyomwezesha kujitegemea kiuchumi na kuboresha maisha yake.
Shalua aliwahimiza vijana wengine wenye ulemavu kutojisikia kunyimwa fursa wala kukata tamaa, bali kutumia mikopo na programu mbalimbali za Serikali kama chachu ya maendeleo yao binafsi na ya jamii kwa ujumla.
“Mkopo huu umebadilisha maisha yangu kwa kiasi kikubwa. Umeongeza kipato changu na kunifanya niheshimike zaidi katika jamii. Serikali imetuwekea mazingira rafiki ya kufanya kazi na kujitegemea, hivyo vijana wenye ulemavu tusibweteke bali tushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi,” alisema Shalua.
Katika ziara hiyo, Ndahani alitembelea Kikundi cha Vijana Blocks kilichopo Kata ya Ndago kinachojishughulisha na ufundi wa ufyatuaji wa matofali, pamoja na Kikundi cha Waoka Mikate cha Malisafi Bakery kilichopo Shelui, ambavyo ni miongoni mwa vikundi vilivyonufaika na fursa za uwezeshaji wa kiuchumi.
Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kufuatilia utekelezaji wa mikopo ya asilimia kumi (10%) inayotolewa kwa vijana na makundi maalum, pamoja na kuhakikisha miradi inatekelezwa ipasavyo, inaendelea vizuri na kuleta tija kwa walengwa na jamii kwa ujumla.
MWISHO
.





Post a Comment