WATUHUMIWA 37 WAKAMATWA KWA TUHUMA ZA MAKOSA MBALIMBALI SINGIDA

Na Sylivester Richard

Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida kupitia operesheni ilizofanya Mwezi Januari, 2025 limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 37 waliojihusisha na makosa mbalimbali ya jinai kwa kipindi cha mwezi Januari 2025. 


Watuhumiwa hao ni pamoja na watuhumiwa 5 waliokamatwa na silaha 5 aina ya gobole bila kibali, watuhumiwa 5 waliopatikana na mali zidhaniwazo kuwa ni za wizi na mtuhumiwa 1 aliyekamatwa na nyara za serikali vipande vinne vya nyama vidhaniwavyo ni vya mnyama aina ya nyati. 


Akiongea kuhusu usimamizi wa Usalama Barabarani Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida SACP Amon Kakwale amesema kuwa makosa 3762 ya Usalama barabarani yalikamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria ambapo makosa 3760 yalitozwa faini na madereva wake kuendelea na majukukumu yao huku madereva wawili  wakifungiwa  leseni zao za udereva kwa miezi 3 kwa kosa la kuendesha gari kwa mwendo kasi usioruhusiwa kisheria.


Aidha, amesema  kuwa kwa kipindi hicho cha mwezi Januari 2025 washitakiwa 51 walihukumiwa vifungo mbalimbali  kutokana na makosa waliyotenda ikiwemo kuhukumiwa kwenda jela maisha kwa Mtuhumiwa mmoja kwa kosa la kubaka.

Post a Comment

Previous Post Next Post