Na Jumbe Ismailly
Igunga,Mkoani Tabora imeanza maandalizi ya kukabiliana na mvua za elinino zinazotarajiwa kuanza akunyesha wakaati wowote mwaka huu,kwa kufukua mifereji pamoja na kusafisha makalvati ili mvua zitakapoanza kunyesha maji yaweze kupita kiurahisi na bila mkwamo wowote.
Meneja wa Wakala wa barabara za Vijijini na Mijini, (TARURA) wilaya ya Igunga,Mhandisi Aswile Mwasaga alisema ili kufanikisha mkakati huo wamepanga pia kuwashirikisha wadau mbali mbali
“Kwa sasa tupo kwenye maandalizi ya kukabiliana na elinino kama inavyosemekana kuwa itaanza mwezi wa kumi,lakini kwa haraka haraka maandalizi tunayofanya kwa sasa hivi tunataka kuanza kufanya shughuli za kusafisha mifereji na kuzibua makalvati ili mvua zikianza kunyesha maji yaweze kupita kwa urahisi bila mkwamo wowote ule” alisisitiza Meneja huyo wa Tarura wilaya ya Igunga.
Alifafanua Mhandisi Mwasaga kwamba ili kufanikisha mkakati huo wamepanga kushirikisha wadau mbali mbali na kwa kuanzia wataanza na wadau wao ambao ni wananchi kwa sababu mifereji mingi imepita kwenye maeneo yao na wao wapo karibu nayo.
“Lakini pia nimeendelea kuwasisitiza na kuwaelimisha kwamba wasitupe takataka kwenye hiyo mifereji kwani takataka huwa zinaziba mifereji na mwisho wa siku zinakwenda kwenye makalvati na maji yanashindwa kupita yanajaa kwenye mifereji baadaye yankuja kupita juu ya barabara,baadaye yanakuja kuvamia makazi ya wananchi” alifafanua
Akizungumzia hali halisi ya barabara za wilaya ya Igunga, Meneja wa Tarura alibainisha kuwa hali ya barabara kwa sasa hivi siyo mbaya sana,kwa madai kuwa zipo barabara wameshazifanyia matengenezo na zipo katika hali nzuri, lakini kulingana na bajeti waliyonayo na kulingana na mahitaji,mahitaji ni makubwa sana kuliko bajeti waliyotengewa.
“Lakini tulikuwa tumejipanga tunakarabati barabara kidogo kidogo kulingana na bajeti yetu inavyokuwa inaruhusu na kwa sasa hivi kuna barabara tumezifanyia matengenezo na zipo katika hali nzuri lakini zipo baadhi ambazo bado hatujazifanyia matengenezo tumeshaziweka kwenye matengenezo ya mwaka ujao wa fedha wa 2026/2027 kwani kwa sasa hivi bado zipo katika hali ya kuridhisha” alibainisha Mhandisi huyo.
Hata hivyo Mhandisi huyo akatumia pia fursa hiyo kutoa wito kwa wakandarasi watakaofanikiwa kupata kazi za kutengeneza barabara kwa kuwataka wajipange vizuri kwa maana ya mitaji lakini pia kwa wataalamu kwani kazi zinazohitajika ni zenye ubora na zenye kutekelezwa kwa kukamilika kwa wakati.
“Wajipange vizuri kwa kutafuta mitaji ya kutosha lakini wawe na timu maalumu ya waataalmu ili kazi iweze kufanyika kwa ubora na kukamilika kwa wakati uliopangwa”alisisitiza Mwasaga.
Kwa upande wao baadhi ya wananchi wa Mjini Igunga, akiwemo mkazi wa Mtaa wa Magereza,Aisha Haruna alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha wananchi wanaokaa kwenye maeneo ya mabondeni waangalie uwezekano kama wa kuhama kabla ya mvua hizo kuanza kunyesha.
“Na kama kuna mitaro iliyoziba ifanyiwe ukarabati au ifanyiwe usafi ili kuepuka madhara yatakayotokana na mvua hizo za elinino”alisisitiza Aisha.
Faridu Salim Abdallah ni mkazi wa Mji mdogo wa Igunga aliendelea kusisitiza serikalini kwamba asilimia 75 ya mifereji ni mizima kwa hali hiyo umefika wakati wa kutilia maanani kwa kuiwekea mkazo wa kuhakikisha mifereji na makalvati yote yanakuwa safi ili mvua zitakapoanza kunyesha maji yaweze kupita bila kukwamishwa na uchafu utakakuwa umeziba madarajani.
“Na kipindi cha nyuma mifereji ilikuwa michafu lakini Halmashauri imejitahidi imechimbisha mifereji baada ya kuchimbisha hata sisi hatukuwa na mifereji katika maeneo tunayoishi,lakini baada ya kutuwekea mifereji tunashukuru maji yanajaa uwani,pembeni mwa nyumba yanaingia kwenye mifereji yanatembea”alisisitiza mwananchi huyo.
MWISHO.

Post a Comment