Na Thobias Mwanakatwe, IRAMBA
WANANCHI wa vijiji vya Ulemo, Kizaga na Misigiri katika Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida, wameipongeza Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kwa kuchukua hatua za kufanya matengenezo katika barabara kuu ya Singida–Igunga mkoani Tabora, wakisema hatua hiyo imewapunguzia adha iliyokuwa ikiwakabili kwa muda mrefu.
Wananchi hao wamesema matengenezo yaliyofanyika katika kipande cha barabara kinachoanzia Kijiji cha Ulemo hadi Misigiri yameleta nafuu kubwa kwa watumiaji wa barabara hiyo, hasa madereva wa magari ya abiria, malori, wafanyabiashara na wananchi wanaosafiri kati ya Mkoa wa Singida na maeneo ya Mkoa wa Tabora.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe, wakati gazeti hili lilipotembelea eneo hilo na kushuhudia hali ya barabara hiyo, wananchi walisema awali baadhi ya maeneo yalikuwa yameharibika kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwepo kwa mashimo yaliyokuwa yakilazimisha magari kupunguza mwendo na wakati mwingine kuyakwepa kwa kuingia upande mwingine wa barabara.
Kwa mujibu wa wananchi hao, hali hiyo haikuwa tu kero kwa watumiaji wa barabara, bali pia ilikuwa ikihatarisha usalama wa abiria na madereva, huku ikiongeza gharama za uendeshaji wa magari kutokana na uharibifu wa matairi, mifumo ya suspension na sehemu nyingine za magari.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Ulemo, Juma Hamisi, alisema kabla ya matengenezo hayo, usafiri katika eneo hilo ulikuwa na changamoto kutokana na hali ya barabara, hasa wakati magari yanapokutana kwenye maeneo yaliyokuwa na mashimo makubwa.
Alisema madereva walilazimika kuwa waangalifu zaidi na kupunguza mwendo ili kuepuka mashimo, jambo ambalo liliongeza muda wa safari na wakati mwingine kusababisha foleni ndogo pale magari yalipokuwa yakikabiliana na mashimo makubwa.
«“Awali barabara ilikuwa na mashimo mengi na makubwa. Dereva akifika hapa alilazimika kupunguza mwendo sana au wakati mwingine kwenda pembeni ili kulikwepa shimo. Hali hiyo ilikuwa inasababisha usumbufu mkubwa kwa magari na abiria,” alisema.»
Alisema tofauti na hali ya awali, kwa sasa magari yamekuwa yakipita kwa urahisi zaidi katika maeneo yaliyofanyiwa matengenezo, huku madereva wakionekana kuwa na uhuru mkubwa wa kutumia barabara bila kulazimika kuyakwepa mashimo kama ilivyokuwa hapo awali.
Mwananchi huyo aliishauri TANROADS kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika barabara hiyo ili kubaini maeneo yanayoanza kuharibika mapema na kuyafanyia matengenezo kabla hali haijawa mbaya.
Naye mkazi wa Kijiji cha Kizaga,Abdullah Omari, alisema hali mbaya ya barabara hiyo ilikuwa ikiwapa wakati mgumu zaidi madereva wanaotumia barabara hiyo mara kwa mara.
Alisema magari yanapopita kwenye mashimo makubwa mara kwa mara, baadhi ya sehemu zake huharibika, hali inayowalazimu wamiliki kutumia fedha nyingi kufanya matengenezo.
«“Mashimo yalikuwa yakisababisha magari kupata hitilafu. Gari linaweza kuingia kwenye shimo na tairi likapata tatizo au sehemu nyingine ya gari kuharibika. Kwa hiyo dereva alikuwa akitumia gharama zaidi kuliko kawaida,” alisema.»
Alisema gharama hizo hazikuwa zikibaki kwa wamiliki wa magari pekee, bali kwa namna moja au nyingine zilimfikia mwananchi wa kawaida kupitia ongezeko la nauli au gharama za usafirishaji wa bidhaa.
Kwa mfano, alisema wafanyabiashara wanaosafirisha bidhaa kwa kutumia magari kutoka Singida kwenda maeneo mbalimbali ya Tabora na kinyume chake walihitaji magari yao yawe katika hali nzuri wakati wote, jambo ambalo lilikuwa gumu endapo barabara ilikuwa na mashimo mengi.
Naye Neeema John alisema matengenezo yaliyofanyika yameanza kuleta mabadiliko yanayoonekana, akieleza kuwa magari sasa yanapita kwa urahisi zaidi katika maeneo yaliyofanyiwa kazi.
«“Sasa tunaona tofauti. Barabara imekuwa nzuri zaidi ukilinganisha na hali iliyokuwa awali. Tunashukuru kwa hatua hii, lakini tunaomba matengenezo yaendelee katika maeneo mengine ambayo bado yana changamoto,” alisema.»
Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Misigiri, Thomas Johnson, alisema hali ya awali ya barabara ilikuwa ikiwapa usumbufu abiria wanaosafiri kwa magari ya abiria na binafsi.
Alisema wakati magari yalipokuwa yakipita kwenye mashimo, abiria walikumbana na mitikisiko mikubwa, hali ambayo ilikuwa ikifanya safari kuwa ngumu na kuchosha.
“Unapokuwa ndani ya gari na linaingia kwenye shimo kubwa, unapata mtikisiko mkubwa. Wakati mwingine abiria walikuwa wakilalamika kwa sababu safari ilikuwa inakuwa ngumu. Sasa hali imeanza kuwa nzuri baada ya barabara kutengenezwa,” alisema.
Alisema barabara nzuri ni muhimu kwa wananchi kwa sababu inaunganisha maeneo mbalimbali na kurahisisha shughuli za kiuchumi, ikiwamo usafirishaji wa mazao, bidhaa na watu.
Aidha, alisema barabara hiyo ina umuhimu mkubwa kwa wakazi wa vijiji vilivyopo kandokando yake kwa kuwa wanaitumia kwenda kwenye masoko, vituo vya huduma za afya, shule na maeneo mengine muhimu.
Wananchi hao walisema matengenezo hayo yamewapa matumaini kuwa changamoto za usafiri zilizokuwa zikijitokeza kutokana na uharibifu wa barabara hiyo zinaweza kupungua ikiwa Serikali itaendelea kuwekeza katika matengenezo ya barabara kwa wakati.
Walisema ni muhimu barabara hiyo kutotunzwa baada ya kuharibika kwa kiwango kikubwa, bali ukaguzi na matengenezo madogo yafanyike mara kwa mara ili kuzuia mashimo madogo kukua na kuwa makubwa.
Mwananchi mwingine wa eneo hilo, Suleiman abdulahaman, alisema uzoefu wa awali umeonyesha kuwa kuchelewa kwa matengenezo kunaweza kuongeza gharama kwa Serikali na wananchi kwa ujumla.
“Ni vizuri barabara ikifuatiliwa mara kwa mara. Shimo likianza leo likarekebishwa mapema, halitakuwa kubwa kesho. Likiachwa linakuwa kubwa, linaharibu magari na baadaye matengenezo yake yanahitaji fedha nyingi,” alisema.
Alisema wananchi wanaunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya barabara, lakini wakaomba matengenezo yafanywe kwa ubora unaoweza kudumu kwa muda mrefu.
Kwa pamoja, wananchi hao waliishauri Serikali kupitia TANROADS kuendelea na matengenezo ya barabara hiyo katika maeneo mengine yenye changamoto, pamoja na kuweka utaratibu wa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara.
Walisema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha barabara inabaki katika hali nzuri na kupunguza uwezekano wa kurudi kwa changamoto za mashimo makubwa zilizokuwa zikisababisha usumbufu kwa watumiaji.
Pia waliomba kuwepo kwa alama za barabarani na tahadhari katika maeneo ambayo bado yanaendelea kufanyiwa matengenezo, ili madereva waweze kuchukua tahadhari na kuepuka ajali.
Kwa upande wa madereva, wananchi hao walisema pamoja na barabara kutengenezwa, bado ni muhimu madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka mwendo kasi na kuwa makini hasa katika maeneo yenye shughuli nyingi za wananchi.
Wananchi walisema barabara ya Singida–Igunga ni miongoni mwa miundombinu muhimu inayochochea shughuli za kiuchumi kwa kuwa inawaunganisha wananchi wa maeneo mbalimbali na kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa.
Walisema wafanyabiashara, wakulima na wafugaji wanategemea barabara hiyo kusafirisha bidhaa na mazao yao kwenda katika masoko mbalimbali.
Kwa wakulima, walisema barabara nzuri hupunguza gharama za usafirishaji na kuwasaidia kufikisha mazao sokoni kwa wakati, wakati kwa wafanyabiashara barabara nzuri huwezesha bidhaa kusafirishwa kwa urahisi na kupunguza gharama zinazoweza kutokana na kuharibika kwa magari.
Kutokana na umuhimu huo, wananchi hao walisema wanatarajia matengenezo yaliyofanyika yawe mwanzo wa hatua endelevu za kuhakikisha barabara hiyo inakuwa katika hali nzuri muda wote.
Walisema endapo barabara itatunzwa vizuri, siyo tu itasaidia kupunguza uharibifu wa magari, bali pia itaongeza usalama wa abiria na kurahisisha shughuli za kiuchumi katika maeneo yote yanayohudumiwa na barabara hiyo.
Kwa sasa, wananchi hao wamesema wanaona tofauti kati ya hali ya awali na hali ya sasa, huku wakisisitiza kuwa matengenezo ya barabara yanapaswa kuwa endelevu na siyo kusubiri barabara iharibike kwa kiwango kikubwa ndipo hatua zichukuliwe.
Wameipongeza TANROADS kwa hatua iliyochukuliwa na kuiomba kuendelea kusimamia ubora wa matengenezo pamoja na kufuatilia kwa karibu maeneo mengine yanayoweza kuanza kuonyesha dalili za kuharibika.
“Tunashukuru kwa matengenezo haya. Tunachoomba sasa ni matengenezo yaendelee na barabara itunzwe mara kwa mara ili tusirudi tena kwenye hali ya mashimo makubwa iliyokuwa ikitupa usumbufu,” alisema Mwanaid Juma



Post a Comment