Na Mwandishi Wetu
Wananchi wa eneo la bondeni katika Kijiji cha Nyakabale mkoani Geita, wanamuomba Waziri Mkuu Dkt Mwigulu Lameck Nchemba aingilie kati mgogoro unaoendelea kati yao na Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) kuhusu mpango wa uhamishaji na fidia.
Wananchi hao wameyasema hayo leo baada ya Mgodi huo mkubwa kabisa Tanzania na Afrika kutamka mbele ya Hashim Komba ambaye ndiye Mkuu wa Wilaya ya Geita kwamba hawana mpango wa kuwalipa wananchi Zaidi ya 135 wanaoishi katika maeneo hayo mkoani Geita.
Awali, katika taarifa iliyowasilishwa kutoka katika Kamati Maalumu ambayo iliundwa na Mkuu wa Wilaya kushughulikia mgogoro huo ambayo taarifa yake amekabidhiwa DC huyo ilisema kwamba GGM hawana nyaraka zozote ambazo zinaonyesha kuwa wameshalipa wananchi wanaoishi katika eneo hilo.
“Hakuna documents zozote ambazo zinaonyesha kuwa eneo hilo limeshalipwa na Mgodi wa GGM. Tumewafuata mara kadhaa watupatie documents lakini hakuna,” taarifa iliyowakilishwa kwa DC alisema hivyo.
Kwa upande wake Afisa Mahusiano Mwandamizi wa GGML Gilbert Mworia alisema kuwa mgodi hauwezi kuwalipa wananchi hao na unakataa mapendekezo ya ripoti iliyowakilishwa kwa kwao na kwa mkuu wa Wilaya ya Geita na tume hiyo maalumu iliyoundwa kushughulikia sakata hilo.
“Hatuwezi kuwalipa wananchi hao fidia, waende kokote wanakojua kupata haki zao,” alisema afisa huyo mwandamizi.
Wakiongea kwa uchungu katika kikao hicho kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya, wakazi wengi wameonyeshwa kusikitishwa na kitendo cha mgodi huo kutaka kuwadhulumu haki zao za msingi.
“Hawa watu wa Mgodi huu kwa kuwa wameamua kutudhulumu haki yetu ya msingi na sisi tumesema hatutatoka katika maeneo yetu, wametufanyia mambo mengi mabaya tumekaa kimya, walifungulia maji ya sumu ambayo waliyatililisha kwenye mto ambapo ng’ombe zetu zilikufa, na wengi wetu walipatwa na matatizo ya kiafya. Halafu hii leo wanakuja na kusema kuwa hawatulipi fidia kwenye maeneo yetu. Kwa hili hatutakubali,” alisema mmoja wa wanakijiji hao katika mkutano huo.
Mwana kijiji mwingine, Shabani L. Shabani alisema: “Ardhi ya bondeni ndiyo ilikuwa tegemeo kuu la maisha kwa wakazi wa Nyakabale. Hapa ndipo tulikuwa tunapopanda mazao na kufuga mifugo midogo ili kujikimu. Ikiwa watatuhamisha kwa nguvu bila malipo ambayo ni haki yetu, sisi hatutakubali kabisa.
Aliongeza, “Tulikaa kimya kwa muda mrefu kwa sababu sehemu hiyo ya bonde baada ya kuanza na vumbi la mgodi, tumekuwa hakuna tena sehemu ya kulima na kufuga.”
Mama Asha, mama wa watoto watatu, anasema usiku haalali kwa sababu anawaza watoto wake watasomea wapi vipi baada ya kuhamishwa kwa nguvu kutoka katika mashamba hayo waliyokuwa wakiyategemea kama chanzo cha uchumi wao.
“Huu sasa umekuwa ni ukandamizwaji kwa sisi masikini na wanyonge ambao hatuwezi kujitetea na hatuna wa kututetea. Tunamuamba Waziri Mkuu aje atusaidie sisi wanyonge tupate haki zetu,” alisema Mama huyo.
Wakati wakazi wengine wakidai kupanga kufunga njia ya kuelekea kwenye mgodi huo kutoka katika kijiji hicho cha Nyakabale, Mkuu wa Wilaya hiyo amewasihi waache kufanya hivyo kwani italeta zogo kubwa hivyo amewaomba mpak kufika siku ya ijumatatu ijayo ataitisha kikao kingine kuangalia uwezekano wa mgogoro huo kupatiwa ufumbuzi.
Wakiongea kwa jazba baada ya Mgodi huo kuikataa ripoti iliyoandaliwa na Kamati hiyo maalumu, wananchi wamesema wataandamana hadi pale watakapolipwa fidia ya maeneo yao. Wanasema uvumilivu wao umefika ukingoni na hawawezi kuendelea kuishi kwa hofu na mashaka kila siku.
Mkuu wa Wilaya ya Geita amesisitiza kuwa hakuna njia ya mkato katika kutatua suala hili zaidi ya maongezi baina ya pande zote. Ameungana na wananchi na kuwaeleza kuwa mambo hayo yanahitaji hekima kubwa ili kuepusha mivutano isiyo ya lazima na kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.
Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa hajakubaliana na msimamo wa mgodi na ametoa muda zaidi kwa pande zote kumaliza kadhia hiyo kwa amani.
Aidha amemuagiza Meneja wa Mahusiano wa GGM kurudisha tena na ripoti kwa ajili ya kutatua tatizo hilo, huku akitangaza kuwa kikao kingine kitafanyika Jumatatu ijayo ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Wananchi sasa wanadai serikali iingilie kati haraka. Wanasema GGM inapata faida kubwa ya dhahabu kila mwaka, hivyo ni haki kwa jamii inayozunguka mgodi pia kunufaika na sio kubakia masikini na kutengwa.
Hadi sasa, bondeni ya Nyakabale bado ni makazi ya watu, lakini ni makazi yenye kutokuwa na uhakika. Kila siku inavyopita hofu inazidi, na shughuli za uzalishaji zimesimama kwa sababu hakuna anayejua kesho yake itakuwaje.
Mwisho wanasema matumaini yao yote sasa yako kwa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu. Wanaamini kama kiongozi wanaosikiliza na kutetea haki za mwananchi wa kawaida, watasaidia kuhakikisha kuwa haki zao zinarejeshwa na mchakato wa uhamishaji unafanyika kwa haki, uwazi na huruma.
Mwisho




Post a Comment