Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya CRJE (East Africa) Ltd imefanya Shindano la kukuza Ujuzi kwa wanafunzi wa Chuo cha Uhandisi na Teknolojia (CoET) cha UDSM. Shindano hilo lilifanyika kupitia _Site Open Day_ katika mradi mkubwa wa Kampuni hiyo uliopo Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Lengo likiwa ni kuhamisha ujuzi kwa vitendo kutoka kwa wataalamu wa Kichina kwenda kwa wanafunzi wa uhandisi wa Kitanzania ili kuimarisha ushirikiano kati ya China na Tanzania.
Kwa mara ya kwanza, wanafunzi wa CoET walitoka kwenye madaftari na slaidi za darasani na kuingia moja kwa moja kwenye uhalisia wa ujenzi. Tukio hilo liliwapa fursa ya kushuhudia ujenzi halisi, usimamizi wa usalama, na utatuzi wa changamoto katika eneo la ujenzi.
Kupitia ziara ya mradi, na shindano la “Nyota wa Baadaye”, CRJE iliweza kuwaonyesha wanafunzi wa uhandisi tofauti kati ya nadharia ya darasani na uhalisia wa kazi. Hii ni hatua inayoziba pengo kati ya taaluma na sekta.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Zhang Cuishan, Naibu Meneja Mkuu wa CRJE, amesema kwa muda mrefu China imekuwa na mahusiano mazuri na Tanzania, hivyo wanaona hii ni fursa ya kuendeleza na kuudumisha uhusiano kati ya nchi hizi mbili kwa kuwasaidia wahandisi wanafunzi kupata ujuzi.
Aliongeza kuwa shindano hilo lina maana kubwa kuelekea 2026. “Mwaka 2026 ni miaka 70 ya uhusiano uliotukuka wa kidiplomasia kati ya China na Afrika. Pia ni ‘Mwaka wa Kubadilishana Kati ya Watu wa China na Afrika.’ Hili si shindano la ujuzi tu, bali mazoezi ya kuvuka tamaduni, kuongeza uelewa, na kuimarisha urafiki,” alieleza.
Alitabanaisha: “Ujuzi ndio msingi wa mafanikio, na vipaji ndio nguzo ya maendeleo. Kupitia shindano hili tunajenga daraja la ujuzi. Wafanyakazi wa Kichina na Kitanzania wanashindana, wanajifunza, na kukua pamoja.”
CRJE ilianza na ujenzi wa Reli ya Tanzania–Zambia na sasa imekuwepo Tanzania miaka 57. “Tumetekeleza zaidi ya miradi 200 ya ubora. Wajenzi wa Kichina wamehamisha ujuzi, Watanzania wengi wamekuwa wataalamu, na vijana wamejiunga nasi,” alisema Bw. Cuishan. “Madhumuni ya shindano hili ni kuhamasisha roho ya TAZARA, umahiri wa kazi, na bidii — kujifunza kwa kushindana na kuboresha ujuzi kwa vitendo.”
Alisema CRJE inataka vipaji vipya vijitokeze, mawasiliano kati ya wafanyakazi kutoka China na Tanzania waweze kubadilishana ujuzi na teknolojia. Pia aliomba ushirikiano wa makampuni na vyuo uimarike ili kukuza vipaji vilivyoko vyuoni. “Vijana wengi zaidi wajifunze kuhusu CRJE na waje kuchangia maendeleo ya Tanzania,” alisisitiza.
Ujuzi na Usalama
Wanafunzi walitembelea maeneo ya kazi na kuona mafundi wa Kichina na Kitanzania wakishirikiana kujenga misingi, kufunga nondo, kumwaga zege, na kupandisha nguzo na sakafu. Waliona pia uendeshaji wa mitambo mizito. Maafisa usalama walieleza matumizi ya PPE na itifaki za kazi. Hivi ni viwango vya CRJE katika kila mradi.
Shindano la “Nyota wa Baadaye” liliwapima washiriki kwa maandishi na vitendo. Walipimwa maarifa ya kiufundi, usimamizi wa miradi, itifaki za usalama na maadili ya kikazi. Majaji walikuwa wahandisi wakuu wa CRJE. Washindi walipata nafasi za intanship na CRJE, zikiunda njia ya moja kwa moja kutoka chuoni kwenda kazini.
Kwa upande wake, Dkt. Innocent Macha, Mkuu wa Chuo cha CoET, aliishukuru CRJE. “Ushirikiano wenu umeongeza umuhimu kwa kivitendo kwa masomo yetu,” alisema. “Huu ni ushirikiano wa kweli kati ya taaluma na sekta.”
Mwaka jana CRJE na CoET walisaini Makubaliano ili kuziba pengo kati ya nadharia ya darasani na vitendo halisi. “Leo naona maono hayo yakitekelezwa. Kujifunza hapa si nadharia bali ni kwa vitendo,” alibainisha Dkt. Macha.
Aliwaambia wanafunzi: “Hii ni fursa ya kujifunza kwenye mradi halisi, kushirikiana na wataalamu, na kushiriki shindano linalopima maarifa na uwezo wa kufikiri.”
*Wanafunzi: “Tumeona Uhalisia”*
Martha Chaula, mwanafunzi wa mwaka wa nne, alisema: “Darasani tunakadiria gharama. Hapa nimeona formani wa Kichina na fundi wa Kitanzania wakifanya kazi kwa pamoja."
Aliongeza: "Tumeweza kujifunza kwa kivitendo yale tuliyofundishwa darasani, ukizingatia pia Kampuni ya CRJE wapo mbali katika suala zima la teknolojia, hivyo tumepata kujifunza mambo mapya zaidi."
Zeynat Said, ambaye naye yupo mwaka wa nne chuoni hapo, alisema kuwa uamuzi wa kampuni hiyo kuwachukua wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo, ni heshima kubwa si tu kwa chuo hicho, bali kwa elimu na maendeleo ya Watanzania kwa ujumla.
Kutoka darasani hadi kwenye tovuti ya ujenzi Mbezi Beach, wanafunzi wa UDSM wamepata ladha halisi ya uhandisi. Na kwa ushirikiano huu, darasa linaanza kujengwa kwa zege.
_Mwisho_



Post a Comment