Na Jumbe Ismailly SINGIDA
WATANZANIA wametakiwa kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo nchini ili kuwawezesha wawekezaji kutoka nje ya nchi kuja kuwekeza kwenye maeneo yao ya karibu na kuongeza upatikanaji wa ajira kwa wataalamu wa fani mbali mbali.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda alitoa wito huo kwenye uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa jengo la zahanati ya Singidani,iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida
Alifafanua kiongozi huyo kwamba mradi huo ambao umekamilika kwa awamu ya kwanza na muda si mrefu huduma za afya zitaendelea kutolewa katika zahanati hiyo kwa ngazi ya zahanati lakini wana mpango wa kuendelea kujenga zaidi hatua ambayo itaiwezesha zahanati hiyo kuwa na sifa za kuwa Kituo cha Afya.
“Lakini kuanzia mwezi Novemba,mwaka huu kwa maelezo yao watakuwa wameanza kutoa huduma na jengo hili litakuwa limekamilika”alifafanua Mwang’onda.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka huu,Mheshimiwa Rais amefanya mapinduzi makubwa sana katika sekta ya Afya,na leo tunakuja kushuhudia kwa mwekezaji wetu ambaye amewekewa mazingira rafiki amekuja kuwekeza Singida,lakini yeye yupo nje ya nchi lakini akaamua Mkoani Singida ni kwa sababu serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Daktari Samia Suluhu Hassani imeweka mazingira rafiki.
“Pengine angeweza kwenda huko kwingine lakini yupo Norway amekuja kuwekeza Singida nyumbani kwa sababu kuna mazingira rafiki,kwa hiyo tunamshukuru sana kwa kuweka mamzingira rafiki kwa wawekezaji lakini hasa katika sekta ya Afya akitaka watanzania wapate huduma za afya kwenye maeneo ya karibu na wanapoishi”alisisitiza Mwang’onda.
Mbunge wa jimbo la Singida mjini,Yagi Maulidi Kiaratu pamoja na mambo mengine alitumia wasaa huo kwa kusema kwamba serikali inatambua na kuthamini jitihada za watu binafsi kwani sekta binafsi ni moja ya sekta ya kujenga uchumi.
“Lakini kipekee nimpongeze champion,kinara wa afya anayefahamika Afrila,Daktari Samia Suluhu Hassan na kwa kukubalika kwake siyo bure ni kwa sababu ameing’ang’ania sekta ya Afya kwa jicho zuri na amekuwa kinara katika kuweka miundombinu ya Afya katika eneo la Kinga,Tiba na tafiti za magonjwa mbali mbali”alifafanua Mbunge Yagi.
Awali akitoa taarifa kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026 ya mradi wa ujenzi wa jengo la zahanati ya Singidani,Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Unyamikumbi,Nuhu Solomon Fute akasema mradi huo utakapokamilika utawanufaisha wananchi 263,841 wa Manispaa ya Singida na Halmashauri za jirani
“Mradi huu ulianza kutekelezwa mwaka 2019 kwa kufuata taratibu zote na umepata vibali vyote kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida na mamlaka nyingine zinazohusika na unatarajia kukamilika ifikapo oktoba,2026 na utekelezaji umefikia asilimia 70” alisisitiza Fute.
Kuhusu gharama za mradi Fute aliweka bayana kuwa mradi huo mpaka utakapokamilika utagharimu kiasi cha shilingi bilioni mbili na mpaka sasa umeshatumia kiasi cha shilingi bilioni 1.2.
Hata hivyo Mganga Mfawidhi huyo aliyataja manufaa ya mradi huo utakapokamilika na kuanza kutoa huduma utahudumia wananchi wapatao 263,841 wa Manispaa ya Singida na Halmashauri za jirani na hivyo kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya na zenye gharama nafuu.
MWISHO
PICHANI Ni Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2026,Wazo Michael Mwang'onda(wa pili kutoka kushoto) akiongea na wananchi waliohudhuria uwekaji wa jiwe la msingi la zahanati ya Singida itakayogharimu shilingi bilioni mbili itakapokamilika kujengwa(Picha Na Jumbe Ismailly)

Post a Comment