GULAMALI APANIA KUMALIZA KERO ZA WANANCHI JIMBO LA ILONGERO

 

Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA



MGOMBEA ubunge wa  Ilongero mkoani Singida kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Haiderali Gulamali, ameahidi kero zinazolikabili jimbo hilo zitageuka historia endapo wananchi watampa ridhaa ya kuwa mwakilishi wao bungeni.



Akizungumza  wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho kwa jimbo hilo uliofanyika katika Kata ya Mtinko, Gulamali, aliwaomba wananchi kuwa na imani naye kwa kumchagua katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini mwezi ujao ili awaletee maendeleo.



“Niwahakikishie nitajenga hoja matatizo ambayo yanawakabili yanakwenda kuwa historia katika jimbo hili, watoto wenu ni watoto wangu, raha zenu ni raha zangu, matatizo yenu ni matatizo yangu  tutakaa pomoja kutatua moja baada ya jingine,” alisema na kuongeza kuwa


“Nitakaa na ninyi mkinikaribisha kwenye nyumba hata ya tembe sio lazima nikae kwenye kiti hata chini, mimi nakaa. Tuko pamoja katika furaha na masikitiko hata msiba nitakuwa na ninyi kila mmoja ataondoka duniani.”



Gulamali, aliwaomba wananchi Oktoba 29, mwaka huu kujitokeze kwa wingi  kumpigia kura nyingi mgombea urais CCM,Samia Suluhu Hassan, wabunge na madiwani wa chama hicho.


“Niwahakikishie siwezi kuwaangusha, kumwangusha rais na viongozi wote wa CCM ambao walikaa wakaniteua niwe mgombea na kuweza kusimama hapa na siwezi kuchezea imani za watu ambazo wamewekeza kwangu,”alisema.



Awali wakati akimnadi mgombea huyo,  Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, aliwataka wananchi waendelee kuwa na imani na chama hicho kwa kuwa ni pekee  chenye uwezo wa kuwaletea maedeleo kupitia wagombea wake.


Alisema Samia katika kipindi kifupi madarakani,  ameleta maendeleo makubwa nchini, hivyo kudhihirisha kuwa ni kiongozi anayefaa na  hakuna sababu kwa wananchio kutomchagua yeye, wabunge na madiwani wa chama hicho.



Kada wa CCM na aliyewahi kuwa Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, alisema kila wananchi mwenye kitambulisho cha kupigia kura, ana wajibu wa kuulinda Mkoa wa Singida kwa kumchagua Samia kwa rais, wagombea ubunge na udiwani wa chama hicho.


Nyalandu, alisema Mkoa wa Singida ambao ni wa CCM ni lazima uchaguzi wa mwaka huu uongoze katika kura za kishindo kwa wagombea wote wa chama hicho.



"Nitasimama pamoja na mgombea ubunge jimbo la Ilongero, Gulamali na kuhakikisha mama Samia anapata kura zote za ndio, naungana na timu ya taifa kwa kutembelea kila mkoa na ndio maana kuna basi pale tunatembea nalo kusaka kura za kishindo za CCM," amesema Nyalandu.


MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post