MAIKO SALALAI AREJESHA FOMU KUGOMBEA UBUNFE JIMBO LA MPWAPWA



Na Lubango Mleka - Mpwapwa, Dodoma. 



Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, amerejesha rasmi fomu ya kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea ubunge wa Jimbo la Mpwapwa katika uchaguzi mkuu ujao.


Akizungumza mara baada ya kurejesha fomu hiyo, Salali ametoa shukrani za dhati kwa uongozi wa CCM ukiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza misingi ya usawa, uwazi na ujumuishwaji katika mchakato mzima wa utoaji wa nafasi za uongozi ndani ya chama.



"Ni heshima kubwa kuona kwamba mchakato huu wa kisiasa umekuwa wa wazi, huru na wa haki, ambapo kila Mtanzania ana nafasi sawa ya kushiriki, bila kujali hali yake ya kimwili au kijamii," alisema Salali.


Amepongeza pia namna chama hicho kinavyoendelea kuwa chombo kinachoendeleza misingi ya usawa kwa vitendo, kwa kutoa fursa kwa makundi yote wakiwemo wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika uongozi na maamuzi ya nchi.



"Nikiwa miongoni mwa watu wenye ulemavu waliowasilisha nia ya kugombea, ninaamini huu ni wakati muafaka kwa jamii kutambua uwezo wa watu wa makundi maalum katika kuleta maendeleo na kuchangia ustawi wa taifa letu," aliongeza.


Maiko Salali anajulikana kwa mchango wake mkubwa katika utetezi wa haki na ustawi wa watu wenye ulemavu, na amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kundi hilo linajengewa mazingira wezeshi ya kushiriki kikamilifu katika nyanja mbalimbali za maisha, ikiwemo siasa.

Post a Comment

Previous Post Next Post