Na Mwandishi Wetu
Singida – Kijana msomi na mtaalamu wa masuala ya udhibiti wa bidhaa za tiba, Japhari Saidi, ametangaza rasmi nia yake ya kuchukua fomu kuomba kuteuliwa kugombea Ubunge wa Jimbo la Singida Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2025.
Akizungumza baada ya kutangaza nia yake, Japhari amesema kuwa ameamua kujitosa katika kinyang’anyiro hicho ili kutoa mchango wake katika maendeleo ya wananchi wa Singida Mjini kwa kutumia uzoefu wake katika utumishi wa umma, taaluma na ushirikiano wa karibu na jamii.
“Ninaamini kuwa Singida Mjini inahitaji mwakilishi mwenye maono mapana, anayejua changamoto za wananchi, na mwenye uwezo wa kushirikiana na serikali pamoja na wananchi katika kuleta maendeleo ya kweli,” alisema Japhari.
Japhari ni mzaliwa wa Kata ya Utemini, Singida Mjini. Ana Shahada ya Kwanza ya Kemia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), na Shahada ya Uzamili ya Sayansi ya Bioteknolojia na Udhibiti wa Bidhaa kutoka Purdue University, Marekani. Kwa zaidi ya miaka 10, amekuwa akihudumu kama Mkaguzi Mwandamizi wa Dawa katika Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), akihusika na usalama na ubora wa dawa katika soko la Tanzania.
Katika hatua za awali, Japhari anatarajia kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo mara baada ya mchakato wa CCM kufunguliwa rasmi, huku akiwasihi wananchi wa Singida Mjini kumpokea kwa moyo wa ushirikiano na kuungana naye katika safari ya mabadiliko chanya.
End
Post a Comment