Na Jumbe Ismailly SINGIDA
HALMASHAURI ya Masispaa
ya Singida itaendelea kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa
kuwawezesha,kuwatia moyo pamoja na kuwahamasisha wananchi wa Manispaa ya
Singida kushiriki katika michezo ili waweze kujiimarisha kiafya na kujikinga na
magonjwa mbali mbali.
Akikabidhi zawadi kwa
washindi wa mchezo wa bao wa kikundi cha mchezo wa bao cha Amani Singida
Mjini,Meya wa Manispaa ya Singida,Yagi Maulidi Kiyaratu amesema kwamba michezo
haina umri wala jinsia na ili kuukuza zaidi mchezo wa bao ameahidi kukiunganisha
kikundi cha mchezo wa bao na wachezaji wa mchezo huo kwenye maeneo mengine ya
Manispaa ya Singida ili waweze kuwa pamoja.
Kwa mujibu wa Yagi mchezo
wa bao una historia kubwa hasa wakati wa kupata uhuru wa Tanzania kwani muasisi
wa taifa hili marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alikuwa akipenda sana
kwenda kucheza bao na wazee ili kupata fursa ya kuongea nao,kuteka busara
zao,kushauriana na hata wakati mwingine kushawishiana namna nzuri ya kuelekea
kupata uhuru.
Hata hivyo Mstahiki Meya
huyo ameweka bayana kwamba suala la michezo lipo kwenye ilani ya uchaguzi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 kwenye eneo la michezo kwani
katika ilani hiyo michezo ni kwa wote bila kujali umri,jinsia rangi wala dini
ya mwanamichezo husika.
Muandaaji wa mashindano
ya kutafuta walimbwende Mkoani wa Singida aliyeshiriki mchezo wa bao,Aunt Bora
Lemmy ametumia fursa hiyo kuwatahadharisha wanawake wengine wanaokwepa
kushiriki mchezo wa bao kwa kuamini kwamba mchezo huo ni wa wanaume peke
yao,kuondokana na dhana hiyo potofu na
badala yake wajenge utamaduni wa kuamini mchezo huo ni kwa wote bila kujali
umri,jinsia,dini na wala kabila la mshiriki..
Akitoa taarifa ya
mashindano hayo ya mchezo wa bao,katibu wa kikundi cha mchezo wa bao cha Amani Singida Mjini,Dr.Philip
Kitundu amefafanua kuwa kati ya timu 17 zilizoshiriki mashindano hayo,timu nne
za mwisho zimeshushwa daraja na hazitacheza ligi katika msimu ujao, na badala
yake zitatakiwa kucheza michezo ya play off (championship),timu mbili
zitakazoshinda zitarudi tena katika ligi kuu na zitakazoshindwa hazitashiriki
kwenye mashindano msimu ujao.
Katibu huyo amewataja
washindi wa mchezo huo wa bao kuwa ni pamoja na Dragoni Ramadhani aliyeshika
nafasi ya kwanza kwa kuwa na alama 38, mshindi wa pili ni Omari Abrahamani
aliyepata alama 35 na mshindi wa tatu ni Chief Sisco Ng;eni aliyepata alama 33.
MWISHO.

Post a Comment