Na Sylvester Richard
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi baada ya kuibuka mshindi wa jumla katika mashindano ya michezo mbalimbali ya Mei Mosi 2025.
Ametoa pongezi hizo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) 2025 yaliyofanyika kitaifa kwenye viwanja vya Bombadia Mkoani Singida.
Aidha Dkt. Samia amewahimiza watumishi wa umma kuhakikisha wanaongeza juhudi katika michezo ili kuwa na afya njema na kuahidi kwamba serikali itakuwa pamoja na watumishi wa umma katika kutatua changamoto zinazowakabili kazini.
Akizungumzia suala la nyongeza ya mishahara kwa watumishi wa umma, Dkt. Samia amesema kuwa kuanzia mwezi Julai 2025 Serikali anayoiongoza itaongeza kiwango cha chini cha mshahara toka kiasi cha Tsh.370,000/= hadi 500,000/= .
Kabla ya hatuba yake Mh. Rais Samia alikabidhiwa zawadi kutoka kwa Shirikisho la wafanyakazi Tanzania kupitia Rais wa Shirikisho hilo Tumaini Mwakyoka kisha yeye kukabidhi zawadi kwa watumishi wa umma waliofanya vizuri 2024.
Naye Katibu wa Michezo Wizara ya Mambo ya Ndani Bi Salma Said Hamza ameishukuru serikali kwa ongezeko hilo la mshahara ambalo amtaja kuwa litaendana na gharama za maisha ya watumishi.
Ametumia nafasi hiyo kuzungumza juu ya ushindi wa pamoja katika michezo ya Mei Mosi na kusema kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani imejinyakulia makombe 11 ikiwemo kombe la Mpira wa Kikapu, Mpira wa Pete, Mpira wa Wavu, Riadha na Bao.
Maadhimisho ya wafanyakazi 2025 kitaifa yamebeba kaulimbiu isemayo " *Uchaguzi Mkuu 2025 Utuletee Viongozi Wanaojali Haki na Maslahi ya Wafanyakazi, Sote tunashiriki"*




Post a Comment