SIGHTSAVERS YAWAPATIA VIFAA WATU 1,830 WENYE CHANGAMOTO YA UONI

 Na Jumbe Ismailly SINGIDA

 


SHIRIKA la Kimataifa lisilo la kiserikali (NGO) la Sightsavers Mkoani Singida limewapatia watu 1,830 wenye kukabiliwa na changamoto ya uoni pamoja na huduma ya upasuaji mdogo wa motto wa jicho na kufanikiwa kuchangia kuondoa upofu unaoweza kuzuilika kwa wananchi wa Mkoa huo.

 

Akitoa taarifa za mradi huo ulianza kutekelezwa katika Halmashauri saba za Mkoa wa Singida tangu mwaka 2023,Mratibu Mradi, Sightsavers Mkoa ni Singida,Upendo Minja alifafanua zaidi ya watu 1,230 wenye changamoto ya uoni walipatiwa huduma za upasuaji mdogo wa mtoto wa jicho na zaidi ya watu 600 walipatiwa huduma ya miwani ili kurekebisha uoni wao.

 

Hata hivyo Upendo aliweka wazi kwamba kupitia utekelezaji wa majukumu yake, shirika hilo limeweza kuhamasisha jamii pamoja na viongozi kuhusu umuhimu wa huduma za afya na haki za watu wenye ulemavu na umuhimu wa ushirikishwaji wao katika maendeleo yaTaifa.

 

“Kwa wenye changamoto za uoni,watu zaidi ya 600 wamepatiwa huduma ya miwani ili kurekebisha uoni wao sambamba na huduma hizo vile vile zaidi ya watu 1,230 wamepatiwa huduma ya upasuaji mdogo wa motto wa jicho na kufanikiwa kuchangia kuondoa upofu unaoweza kuzuilika kwa wananchi wa Mkoa wa Singida”alisisitiza Mratibu huyo wa mradi.

 

Mratibu huyo wa mradi alibainisha kwamba shirika hilo linafanyakazi na serikali, mashirika ya kiraia pamoja na jamii ili kuboresha huduma za afya ya macho, kuwezesha watu wenye ulemavu kupata haki zao na kusaidia maendeleo ya kiuchumi.

 

Hata hivyo Upendo aliweka wazi kwamba kupitia utekelezaji wa majukumu yake, shirika hilo limeweza kuhamasisha jamii pamoja na viongozi kuhusu umuhimu wa huduma za afya na haki za watu wenye ulemavu na umuhimu wa ushirikishwaji wao katika maendeleo yaTaifa.

 

Aliweka bayana kuwa katika kutekeleza jitihada za maendeleo kwa wananchi, Mkoa wa Singida chini ya serikali ya awamu ya sita ya Mama Samia Suluhu Hassani umeweka mazingira wezeshi kwa wadau kuweza kutekeleza miradi ya maendeleo ya Mkoa wa Singida.

 

“Mmoja wa wadau wanaoshirikiana na Mkoa wa Singida ni shirika la Sightsavers lenye dhima ya kutoa huduma endelevu za afya ya macho kwa wananchi na kutetea haki ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika Mkoa wa Singida” alisisitiza mratibu mradi huyo.

 

Hata hivyo aliweka bayana kwamba kutokana na mazingira hayo wezeshi, Sightsavers husaidia kufanikisha huduma za afya ya macho kwa watu walioko vijijini pamoja na maeneo ya pembezoni ili kufikia adhima ya serikali ya huduma bora za afya.

 

Kwa mujibu wa mratibu mradi huyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Mheshimiwa Raisi Daktari Samia Suluhu Hassani,Shirika hilo la Sightsavers kuanzia mwaka 2023 mpaka sasa linaendelea kutekeleza mradi wa Macho Yangu katika Halmashauri saba za Mkoa wa Singida.

 

Alifafanua kuwa mradi huo umeweza kufikia wananchi katika utoaji wa huduma za upimaji na uchunguzi wa afya ya macho,utoaji huduma za miwani kwa lengo la kurekebisha uoni pamoja na upasuaji mdogo wa motto wa jicho.

 

“Takwimu zinaonyesha watu zaidi ya 18,000 wamepata huduma ya uchunguzi wa macho kupitia vituo mbali mbali vya afya pamoja na huduma mkoba zinazofanywa kwa ajili ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

 

Aidha Upendo alibainisha kuwa katika utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa uchumi kwa watu wenye ulemavu,Shirika la Sightsavers kwa kushirikiana na Mkoa limefanya hamasa kwa watu wenye ulemavu kujiunga na shughuli za kilimo cha mtama, kufanya mafunzo ya ujasiriamali na kujiajiri, hususani kwa vijana.

 

Alifafanua pia kwamba idadi ya vijana wapatao 50 kutoka sehemu mbali mbali za Mkoa wa Singida wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na kujiajiri na watu wenye ulemavu wapatao 30 wamepatiwa mafunzo ya kilimo bora cha mtama katika Halmashauri ya wilaya ya Mkalama.

 

Hata hivyo Upendo aliweka bayana pia kuwa ili vijana pamoja na watu wenye ulemavu wawezeshwe kushiriki katika kuchangia shughuli za kiuchumi, Sightsavers waliweza kugawa vifaa saidizi kulingana na mahitaji kwa watu wapatao 11 na kuchangia mitaji kwa vijana watano wenye ulemavu kwa kuwapatia vifaa vya kuongeza mitaji yao.

 

Alivitaja vifaa hivyo kuwa ni pamoja na mitungi ya gesi, mashine ya kushonea, masweta, cherehani pamoja na bidhaa za dukani kama chachu ya kuhamasisha wadau wengine kuweza kufanya kazi na makundi hayo maalumu.

 

MWISHO.

 

Post a Comment

Previous Post Next Post