HALMASHAURI YA WILAYA YA SINGIDA KUTUMIA ZAIDI YA BILION 17.7 UJENZI WA BWAWA LA UMWAGILIAJI

 Na Jumbe Ismailly SINGIDA

 


HALMASHAURI ya wilaya ya Singida inatarajia kutumia shilingi milioni 17,705,174,240/=  kukamilisha ujenzi wa bwawa la umwagiliaji katika Kata ya Msange,wilayani Singida  lenye ukubwa wa hekta 1,000.

 

Akielezea mafanikio ya Idara ya Kilimo,Mifugo na Uvuvi kwa kipindi cha mwaka wa fedha wa 2021/2022 hadi mwaka 2023/2024, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Singida,Elia Mlangi Digha alisema Halmashauri hiyo inajihusisha na kilimo cha umwagiliaji kinachofanyika katika maeneo yenye mabonde na maeneo yanayofaa kwa ajili ya kilimo cha kumwagilia.

 


Aidha Digha ambaye pia ni diwani wa Kata ya Msange alifafanua kuwa wataalamu wa umwagiliaji walibaini maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji yenye ukubwa wa hekta 5,157 yanayofaa kwa uchimbaji wa visima kwa lengo la kufanya shughuli za kilimo, hususani wakati wa kiangazi.

 

Akifafanua zaidi Mwenyekiti huyo alisema katika kipindi cha miaka mitatu serikali pia imeidhinisha ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji katika kata ya Mughamo na Msange.

 

“Halmashauri imewezeshwa ujenzi wa bwawa la umwagiliaji katika Kata ya Msange ambapo eneo la umwagiliaji lina ukubwa wa hekta 1,000 na mradi unagharimu jumla ya shilingi 17,705,174,240/= ambapo shughuli za ujenzi zinaendelea.

 

Akizungumzia usajili wa wakulima kwenye mfumo wa TFRA,Digha aliweka wazi kwamba Halmashauri ya wilaya ya Singida imefanikiwa kusajili kwenye daftari wakulima 42,766 na kuwaingiza kwenye mfumo wa TFRA wa mbolea za ruzuku ili kuhakikisha wanapata namba za kuwawezesha kupata mbolea na mbegu za ruzuku.

 

“Halmashauri ilikuwa na lengo la kusajili wakulima 42,766 kutoka katika vijiji vyote 84,hadi sasa tumesajili wakulima wote kwa asilimia 100 na zoezi la usajili linaendelea”alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Halmashauri ya wilaya ya Singida.

 

Halmashauri ya wilaya ya Singida ina eneo la kilomita za mraba 5,053 ambazo kati ya hizo,eneo linalofaa kwa kilimo ni kilomita za mraba 3,214 na kilomita za mraba 1,839 zinazobaki ni kwa ajili ya eneo la malisho,misitu,maji,maziwa na mito na eneo kwa ajili ya madini,vilima pamoja na mawe.

 

MWISHO.

Post a Comment

Previous Post Next Post