KILIMO IKOLOJIA NI NJIA YA UHAKIKA YA KUIMARISHA MIFUMO YA CHAKULA AFRIKA MASHARIKI

Na Daudi  Manongi

Katika juhudi za kuimarisha mifumo ya chakula Afrika Mashariki, wadau wa kilimo kutoka nchi mbalimbali walikutana jijini Nairobi, Kenya, katika *Mkutano wa Pili wa Afrika Mashariki wa Kilimo Ikolojia*, uliofanyika kuanzia Machi 25 hadi 28, 2025. Mkutano huo uliandaliwa na Biovision Africa Trust kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo ya Kenya, na kushirikisha zaidi ya washiriki 700 kutoka sekta mbalimbali, wakiwemo wataalamu wa kilimo, wakulima, watunga sera, vijana, wanawake, na mashirika ya kiraia.


*Tanzania Yaweka Alama*

Tanzania ilitoa mchango mkubwa kupitia ushiriki wa taasisi na mashirika mbalimbali yaliyo mstari wa mbele katika kuendeleza kilimo ikolojia. Miongoni mwa washiriki wa Tanzania walikuwemo:  

- Tanzania Alliance for Biodiversity (TABIO)  

- Msonge Organic Farm  

- Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA)  

- The Agroecology Hub Tanzania  

- Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia (NM-AIST)  

- PELUM Tanzania  

- Sustainable Agriculture Tanzania (SAT)  

- Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM)  

- The Kilimanjaro Permaculture Community  

- Biodifenders Ltd  

- Islands of Peace (IDP - Tanzania)  

- SWISSAID Tanzania


Mashirika haya yaliwasilisha uzoefu wa Tanzania katika kuhimiza mbinu endelevu za kilimo, kushirikisha jamii, kulinda rasilimali asilia, na kuendeleza mifumo ya chakula inayojali afya ya binadamu na mazingira.



*Ujumbe wa Mtaalamu: Tuondoke Kwenye Karatasi, Tuingie Vitendo*


Miongoni mwa waliochangia mijadala ya kitaalamu ni **Daud Ngosengwa Manongi**, mtaalamu wa kilimo ikolojia kutoka Tanzania, ambaye alisisitiza kuwa wakati umefika kwa serikali za Afrika Mashariki kuanza kutekeleza mikakati waliyoipitisha kuhusu kilimo ikolojia badala ya kuendelea kuizungumzia tu kwenye makongamano.


> *“Tuna sera nzuri, tuna ramani za njia, tuna mipango ya utekelezaji—lakini bado utekelezaji mashinani ni hafifu. Kilimo ikolojia siyo tena jambo la kujadili, ni jambo la kutekeleza sasa,”* alisema Ngosengwa.


Ngosengwa pia alielezea matokeo ya utafiti wa TAPE (Tool for Agroecology Performance Evaluation), akibainisha kuwa ushahidi wa kitaalamu unaonyesha kuwa kilimo ikolojia ni suluhisho bora katika:  

- Kukabiliana na changamoto ya uzalishaji mdogo kwa kutumia mbinu rafiki kwa mazingira,  

- Kulinda bayoanuai ya mazao na mifumo ya ikolojia,  

- Kuimarisha uchumi wa wakulima wadogo kupitia gharama nafuu na tija kubwa,  

- Kuweka msingi wa afya bora kwa walaji kwa kuwa chakula kinachozalishwa hakina kemikali hatarishi.

> *“Takwimu za TAPE zinaonesha kuwa mashamba ya kilimo ikolojia yanaweza kuwa na tija kubwa, huku yakitunza ardhi na afya ya walaji. Kilimo hiki ni uhalisia, siyo nadharia,”* aliongeza.


*Kilimo Ikolojia: Suluhisho la Jumla*


Mkutano ulisisitiza kuwa kilimo ikolojia siyo tu mbinu ya kilimo, bali ni mfumo mpana wa maisha unaoleta usawa wa kijamii, ulinzi wa mazingira, ustawi wa kiuchumi na afya kwa jamii. Wadau walisisitiza kuwa mafanikio hayawezi kufikiwa bila kuweka mazingira wezeshi, ikiwa ni pamoja na:  

- Uwezeshaji wa sera na sheria zinazotambua kilimo ikolojia,  

- Upatikanaji wa fedha na mikopo rafiki kwa wakulima,  

- Mafunzo na uhamasishaji wa vijana na wanawake,  

- Utafiti na ushahidi wa kisayansi,  

- Ulinzi wa mbegu asilia kama msingi wa uhuru wa chakula.


*Wito kwa Vyombo vya Habari vya Tanzania*


Mkutano pia ulihitimishwa kwa wito maalum kwa vyombo vya habari Tanzania kuwekeza nguvu katika kuripoti kwa kina masuala ya kilimo ikolojia.


> *“Vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kufikisha ujumbe kwa jamii, kuwahamasisha wakulima na kushawishi watoa maamuzi. Tunahitaji magazeti, redio, TV na mitandao ya kijamii kueleza kwa kina faida za kilimo ikolojia. Ni kwa njia hii tunaweza kufanikisha mabadiliko ya kweli,”* alisema Ngosengwa.




Tanzania ina hazina kubwa ya uzoefu, taasisi makini, wataalamu waliobobea, na wakulima walio tayari kufanya kazi kwa vitendo. Kwa kuunganisha nguvu na kushirikisha wadau wote—kutoka serikali hadi mashinani—kilimo ikolojia kinaweza kuwa mhimili wa uchumi wa vijiji, ulinzi wa mazingira, na afya ya Taifa.

Post a Comment

Previous Post Next Post