Na Jumbe Ismailly SINGIDA
MKOA wa Singida una jumla
ya wafugaji nyuki 15,326 wakiwemo wanaume 12,377 na wanawake 2,949 wanaozalisha
zao la asali katika mapori na misitu iliyopo katika Halmashauri saba zilizopo
katika Mkoa huo.
Afisa Maliasili wa
sekretarieti ya Mkoa wa Singida,Charles Kidua alitoa takwimu hizo alipokuwa
akitoa taarifa ya mazao yanayotokana na nyuki katika Mkoa wa Singida.
Aidha afisa huyo mwenye
dhamana ya kusimamia sekta ya maliasili alifafanua kwamba Halmashauri ya Itigi
inaongoza kwa kuwa na wafugaji 5,012 wakiwemo wanaume 4,030 na wanawake 982.
Kwa mujibu wa Kidua
Halmashauri ya wilaya ya Ikungi ina wafugaji nyuki 3,841 wakiwemo wanaume 2,636
na wanawake 1,205 wakati Halmashauri ya wilaya ya Manyoni ina jumla ya wafugaji
nyuki 1,934 wakiwemo wanaume 1,876 na wanawake 78.
Hata hivyo afisa
maliasili huyo alibainisha pia kuwa Halmashauri ya wilaya ya Iramba ina jumla
ya wafugaji nyuki 1,562 wakiwemo wanaume 1,241 na wanawake 321 na Halmashauri
ya wilaya ya Singida ina jumla ya wafugaji nyuki 1,232 wakiwemo wanaume 1,016
na wanawake 216.
Kwa upande wa Halmashauri
ya Mkalaama ina jumla ya wafugaji nyuki 905 wakiwemo wanaume 812 na wanawake 93
na Halmashauri ya Manispaa ya Singida ina jumla ya wafugaji nyuki 820 wakiwemo
wanaume 766 na wanawake 54 na kuzitaja wilaya zenye vituo vya kusindika asali
kuwa ni wilaya ya Singida na wilaya ya Manyoni.
“Wilaya zenye kituo cha
kusindika asali ni wilaya ya Singida yenye viwanda viwilio kikiwemo cha SIDO
Mkoa,Kijiji cha nyuki kilichopo Kijiji cha Kisaki,Manispaa ya Singida na wilaya
ya Manyoni kiwanda cha Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS)”alisisitiza
Kidua.
Akizungumzia soko la
asali inayopatikana Mkoa wa Singida,Kidua alisema kwamba asali hiyo huuzwa
katika mikoa ya Manyara,Arusha,Dodoma pamoja na mkoa wa Dar-es-Salaam.
MWISHO.

Post a Comment