MKOA WA SINGIDA WAVUNA ZAIDI YA TANI 334.9 ZA MAZAO YA NYUKI

 Na Jumbe Ismailly SINGIDA            


MKOA wa Singida umevuna tani 334.99 za mazao ya nyuki zikiwemo tani 296.4 za asali na tani 38.95 za nta katika cha kipindi cha kuanzia mwaka 2024 na 2025 huku Mkoa huo unakadiriwa kuwa na mizinga ya kienyeji ipatayo 151,022 na mizinga ya kisasa 12,076.

Akitoa taarifa za ufugaji nyuki katika Mkoa wa Singida,Afisa maliasili wa Mkoa wa Singida,Bwana Charles Kidua amesema sekta hiyo imejikita katika kukuza uchumi kwa kuimarisha na kuongeza upatikanaji wa  mazao ya nyuki ikiwemo asali pamoja na nta.

Kuhusu mazingira na mabadiliko ya taibianchi,Bwana Kidua ameweka bayana kwamba Mkoa wa Singida kama ilivyo mikoa mingine haujaachwa katika kupata madhara ya mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Afisa maliasili huyo Mkoa umekumbwa na ongezeko la joto pamoja na mtawanyiko mbaya wa mvua,hali inayopelekea kupata upungufu wa chakula na magonjwa yatokanayo na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi yakiwemo magonjwa ya mtoto wa jicho na mengine mengi.

Hata hivyo afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya maliasili amebainisha kuwa Mkoa huo umejaaliwa kuwa na madini ya aina mbali mbali yakiwemo dhahabu,chumvi,shaba,jasi,madini ya ujenzi  na vito vikiwemo quarts  na Amethysts.

Akizungumzia sekta ndogo ya wanyamapori amesema Mkoa una mapori ambayo ni makazi mazuri ya wanyamapori na mapori hayo yamegawanyika katika sehemu kuu mbili,ambayo ni mapori ya akiba yanayomilikiwa na serikali kuu na mapori ya hifadhi ya ardhi za vijiji.

Hata hivyo Bwana Kidua ameyataja mapori hayo kuwa ni pamoja na Rungwa,Muhesi na Kizigo yaliyopo katika wilaya ya Manyoni ambayo yana idadi kubwa ya tembo ukilinganisha na mapori mengine ndani ya nchi na yanatumika kwa uwindaji wa kitalii,yakiwa na vitalu vya uwindaji ndani yake.

MWISHO.

Post a Comment

Previous Post Next Post