MKOA WA SINGIDA KUPANDA MITI 10,500,000 KILA MWAKA

 Na Amini Nyaungo, SINGIDA

MKOA wa Singida umejiwekea malengo ya kupanda jumla ya miti 10,500,000 sawa na miche ya miti 1,500,000 kila mwaka kwa kila Halmashauri iliyopo katika Mkoa huo.


Afisa maliasili wa Mkoa wa Singida,Bwana Charles Kidua hata hivyo amesema kwamba kutokana na uwepo mkubwa wa mabadiliko ya tabianchi na bajeti za kila mwaka,Mkoa wa Singida umeweza kufikia malengo ya upandaji miti kwa asilimia 40.35 katika kipindi cha miaka mitatu.

Amebainisha afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya maliasili kuwa mkoa wa Singida umefanikiwa kupanda miti 11,064,135 ambapo kwa mwaka 2024 umepanda miti 5,040,375 na mwaka 2025 miti 6,923,805 sawa na asilimia 52.68 ya utekelezaji.

Akifafanua zaidi idadi ya miche ya miti iliyopandwa katika kipindi cha kuanzia mwaka 2024 hadi mwaka 2025,afisa maliasili huyo amesema kuwa mwaka 2024 Halmashauri ya wilaya ya Manyoni imepanda miti 578,000 wakati mwaka 2025 miche ya miti 738,285 na hivyo kufanya jumla ya miche ya miti 816,285 sawa na asilimia 27.21 ya utekelezaji.

Aidha Bwana Kidua amebainisha pia kuwa kwa Halmashauri ya Itigi imepanda miche ya miti 1,056,000 kwa mwaka 2024 na mwaka 2025 miche ya miti 1,086,496 na kufanya jumla ya miche ya miti 2,142,496 sawa na asilimia 4.75 ya utekelezaji.

Kwa Halmashauri ya wilaya ya Iramba jumla ya miche ya miti 1,831, 327 imepandwa ikiwepo miti 678,098 iliyopandwa mwaka 2024 na miti 1,153,229 ilipandwa mwaka 2025 ambayo ni sawa na asilimia 61. 04 ya utekelezaji.

Kwa mujibu wa afisa maliasili huyo wa Mkoa wa Singida jumla ya miti 1,775,123 imepandwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Singida ikiwemo miti 660,000 iliyopandwa mwaka 2024 na mwaka 2025 imepandwa miti 1,215,123 sawa na asilimia 59.17 ya utekelezaji.

Hata hivyo ameweka wazi kuwa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi imepanda miti 640,000 mwaka 2024 na mwaka 2025 miti 678,000 na kufanya jumla ya miti 1,018,000 sawa na asilimia 33.93 ya utekelezaji.

MWISHO.

Post a Comment

Previous Post Next Post