Na Sylvester Richard.
Madereva wanaoendesha vyombo vya usafiri wakiwa wamelewa wamepatiwa mwaarobaini baada ya mdau wa Usalama Barabarani Praygod Joramu Tarimo ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya FC Enterprise (2002) ya Singida kukabidhi vifaa viwili vya kisasa vya kupima ulevi kwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida.Akipokea vifaa hivyo Januari 17, 2025 nje ya Jengo la Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Singida, Kamanda wa Polisi mkoani humo SACP Amon Daudi Kakwale kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Camillus Mongoso Wambura amemshukuru mdau huyo kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha usalama barabarani na kufanya maamuzi ya kununua vifaa hivyo ambavyo vitasaidia kuwabaini madereva wanaoendesha vyombo vya usafiri wakiwa wamelewa.
Aidha, Kakwale amemwelekeza Mkuu wa Usalama Barabarani Singida(RTO) Mrakibu wa Polisi (SP) Robert Sewando kuhakikisha anasimamia vyema matumizi sahihi ya vifaa hivyo ili madereva walevi wakamatwe na kuepusha ajali hivyo kutekeleza wajibu wa Jeshi la Polisi wa kulinda usalama wa raia na mali zao.
Naye Praygod Joramu Tarimo mdau aliyejitolea vifaa hivyo amesema kuwa ameguswa na ajali za barabarani zinazotokea zinazosababishwa na madereva walevi hivyo kuamua kununua vifaa hivyo ili madereva wapimwe na wanapobainika kuendesha wakiwa wamelewa wachukuliwe hatua kama sheria za usalama barabarani zinavyotaka.
Wakati huo huo Tarimo ameahidi kununua vifaa vingine zaidi na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kumuunga mkono katika kuliwezesha Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani kwa lengo la kukomesha ajali katika Mkoa wa Singida.Mwisho
Post a Comment