HABARI

MICHEZO

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

HABARI

HABARI

MAKALA

» » RAIS SAMIA AMETUUMBUA KAPIGA KATIKA MSHONO


Na Amini Nyaungo

Wakati nimeketi ukumbini kwangu kuangalia Televisheni ufunguzi wa kongamano la Waandishi wa Habari wakiwa na Rais Daktari Samia Suluhu Hassan lililofanyika jijini Dar es Salaam nimepata faraja mpya kabisa katika moyo wangu. 

Kuna wimbi la Waandishi wa Habari wamekata tamaa katika fani hii kutokana na madhira yanayopatikana ndani yake, moja ya hayo ni kuteswa na waajiri kunyanyaswa na kutopata mishahara kwa wakati. 
Rais Samia Suluhu Hassan ametuumbua na kupiga katika mshono kwa wanahabari kwa kutuambia ukweli kwa kusema mabaya ya wenzetu wakati yale yanayotusibu hatuyasemi, namnukuu aliposema ya kuwa "Kuna muda nilichelewa kutoa mishahara kwa siku moja tu lakini habari zilizotoka sasa, Samia hajatoa mishahara, "

Naunga mkono hili kutoka kwa Rais wangu ambaye amekuja kutupa mwanga na uhuru halisi wa kutoa na kusambaza habari . 

KWANINI KAPIGA KATIKA MSHONO ? 

Wanahabari tunahali mbaya sana katika maisha yetu ya kila siku, hatuna mishahara yenye kuendeleza maisha yetu,  hatuna mikataba na kuacha kazi hatuwezi maana tukiacha familia zetu zitaenda wapi ? Ndio maana unamkuta mwanahabari kapita vyombo vya habari 10 au zaidi yote hayo anatafuta maslahi yaliyobora.
Wanahabari tunakaa miezi mitano hadi sita hatujaona mshahara wa ofisi tunazofanyiakazi, hii sio kwa chombo kimoja bali karibuni vyombo vyote hapa nchini, kwa wale wanaofanyiakazi Azam Media na TBC wao angalau tunaambiwa wanaishi kifalme ila zilizobaki tabu iko pale pale.

Mikoani ndio kabisa tia maji tia maji pangu pakavu, huu ndio ukweli ambao wanahabari tunaupitia ila hatusemi ukweli kazi yetu umbea na kushadadia maslahi ya wenzetu.

Ofisini kwetu tunadharauliwa sana huku muajiri anataka habari motomoto hali ya kuwa hajalipa mshahara kwa wakati.

BAHASHA NI NINI ?
Ukweli tuseme Wanahabari tunategemea bahasha ili tuishi na hizi bahasha zisingekuwepo basi nasisi tungerudi kulima tu.

Bahasha zinatolewa na "Source" nimeificha hivyo ili msijue zaidi siri zetu ila huyu "Source" ni mtu muhimu sana kuliko mwajiri huo ndio ukweli najua hii tutakorofishana sana na wanahabari wenzangu.

"Source" ni yule anayekuita katika habari yake baada ya kufanya yale yanayomuhusu basi anatoa posho na kazi inaendelea.

Niliwahi kubahatika kufanyakazi katika vyombo vya nje huwa wanakataza kabisa kuchukua  bahasha wanakwambia ukimaliza njoo ofisini uandae habari uitoe, wanafanya hivi wenzetu wanatoa kila kitu yaani mwandishi anajitosheleza na mshahara pamoja na posho kwa vyombo vya kimataifa.
"Source" muishi miaka mingi, ila sijui kama ni rushwa au ni nini , lakini kipekee apongezwe Mkuu wa mkoa wa Mwanza aliwahi kutujali na kauli na kuona umuhimu wetu.
WAAJIRI KUTOKUWA NA LUGHA NZURI
Hawa waajiri wetu wanalugha chafu sana yaani msituone  huko nje tunatabasamu na kupendeza kwa kuwa watanashati lakini wenzenu tunachambwa huku na mabosi zetu na ukiangalia huna namna inabidi uvumilie tu kwa maslahi ya familia yako.

Ukimjibu  bosi wako anaona unamdharau basi wewe utaandamwa hapo ofisini hadi ukimbie na anasubiri uache kazi ili atumie pesa kukudhulumu haki yako ambayo unayomdai , kwakuwa ana wanasheria ana pesa ya kuwalipa wewe hauna basi haki yako inaenda na maji.
Hili nalo serikali mliangalie kwa ukubwa wake tunaumia sana kwa kazi tunayofanya ndio maana tukipata habari mbaya tunawakanda kweli kweli wakati mwingine sio weledi bali hasira za kutolipwa shuruba na dharau za mwajiri baba mwenye nyumba anadai kodi vyote vinaungana habari itakayo toka hapo ni bomu la Heroshima.
SABABU YA MAUDHUI  MABAYA MTANDAONI 
Hii inawezekana kutokuwa sawa kiakili kwa manaa ya hayo niliyoyaeleza ndio sababu ya kuanika vitu vibaya mtandaoni. 

KAULI YA KISHUJAA NA YAFARAJA KUTOKA KWA SAMIA
Baada ya maelezo yote Rais Samia amepigilia msumari ya kuwa Waajiri wawalipe wanahabari stahiki zao huku akisisitiza habari zenye uchambuzi ndani yake. 

Madeni ambayo wamiliki wa vyombo vya habari wanaidai serikali yenye ushahidi yatalipwa na amesisitiza yalipwe ndani ya mwaka huu kabla ya Disemba. 

HALI YA UHURU WA VYOMBO VYA HABARI VIKOJE ? 
Ni kweli kama upo katika tasnia hii miaka 5 nyuma na miaka 5 ya sasa kuanzia 2021 hadi 2024 unaweza kuona mwanga umekuwa mkubwa uhuru upo na unatekelezwa kwa vitendo. 

Mimi nina miaka 13 sasa katika fani hii tangu nianze 2011 hadi leo najua tulipotoka hadi tulipo, miaka 5 nyuma mimi nilikuwa nalazimishwa kuandika makala kumsifia kiongozi flani hata kama sioni zuri alilofanya lakini pia chombo kikiandika au kufichua madudu ya serikali basi kitakuwa matatani kufungiwa. Ila sasa uhuru tunao na tunapigakazi kama kawaida.  Sio uhuru tu bali tunaweza kujieleza na kuongea chochote juu ya serikali jaokuwa tusivuke mipaka tu na hakuna kutekwa wala kufungiwa chombo cha habari.

Kwa jambo hili apongezwe Rais Samia kwa kazi nzuri anayoifanya pamoja na kuipa hadhi tasnia yetu. 

OMBI LA WANAHABARI
Tasnia hii inasemwa kuwa muhimili wa nne unaojitegemea kwanini wabunge wasipitishe hili iwe kweli kuwa muhimili wa nne  baada ya ile mitatu ya Serikali, Bunge na Mahakama, kwa sababu hao wote wanategemea wanahabari na vyombo vyake ili habari zao sisikike. 

USHAURI WANGU KWA WANAHABARI
Ukweli ni kwamba tumekuwa wavivu kuandika habari za kichambuzi japo tatizo nimelisema huko juu ila inatubidi tuwe na uchungu na kazi zetu tuumize vichwa katika kuandika na kutoa habari nzuri. 

Wanahabari tutumie vizuri maandishi yetu katika kulitetea taifa letu. 

Mwisho. 

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply