HABARI

MICHEZO

Theme images by kelvinjay. Powered by Blogger.

HABARI

HABARI

MAKALA

» » TAHOSA KANDA YA KATI YABAINISHA CHANGAMOTO ZINAZOKWAMISHA UFAULU

 

Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA 

UMOJA wa Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSA) Kanda ya Kati, umesema shule mpya kucheleweshewa fedha za ruzuku na ushirikiano hafifu wa wazazi katika kuchangia chakula cha wanafunzi mashuleni kunasababisha ufaulu usioridhisha katika shule.

Mwenyekiti wa TAHOSA Kanda ya Kati,Jeremia Mungwe, amebainisha hayo jana (April 22,2024) wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa umoja huo unaofanyika katika Manispaa ya Singida na kuwashirikisha wakuu wa shule zaidi 400 kutoka Mikoa ya Dodoma na Singida.

Wakuu hao wa shule wamekutana ili kufanya tathimini ya hali ya elimu pamoja na kupeana uzoefu katika taaluma katika wilaya ambazo zinafanya vizuri kielimu kwa lengo la kuongeza ufaulu katika shule.

"Tunampongeza rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya katika uboreshaji wa elimu, hata hivyo kuna changamoto tunazokumbana nazo mfano shule mpya zinacheleweshewa ruzuku hivyo uendeshaji unakuwa mgumu," amesema Mungwe.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego,akifungua mkutano huo amesema kanda ya kati bado haifanyi vizuri kielimu hivyo ni wajibu wa TAHOSA kujadili tatizo hilo na kutoa mapendekezo kwa serikali nini kifanyike ili kuinua kiwango cha ufaulu katika mikoa ya Singida na Dodoma.

"Kila mmoja anatambua kazi kubwa anayofanya rais Samia Suluhu Hassani na serikali yake kwa kujenga shule mpya,mabweni na vyoo kwa wingi,kwa haya yanayofanyika ina maana serikali inakwenda na muda hivyo ni jukumu lenu na nyie walimu kuongeza ufaulu katika shule," amesema Dendego.

Amesema wakuu wa shule wasiwe wanakaa na madeni ya walimu kinachotakiwa wakiyapokea wayapeleke katika ngazi zinazohusika ili walimu waweze kulipwa haki zao kwa wakati na hivyo kupata morali ya kufanya kazi yao vizuri.


"Msikumbatie matatizo yale ambayo ni changamoto tuleteeni mimi sina urasimi kwenye suala la maendeleo na hivi sasa wakuu wa shule wawe wanaitwa kwenye Vikao vya Maendeleo ya Kata (WDC) ili kusaidia kuleta maendeleo," amesema Dendego.

Amesema wakuu wa shule ambao wamesomea masomo ya sayansi kama Hesabu,Bailoji na Fizikia watoke maofisini na kwenda kufundisha madarasani kwa sababu kuna upungufu mkubwa wa walimu katika masomo hayo.

"Kiongozi ni kuonyesha njia, ukiona mwalimu wako pengine hayupo katika hali yake ya kawaida unamwita unaongea naye kujua tatizo lake na ikiwezekana unampa hata off siku mbili akae sawa maana walimu nao wanachangamoto zao zikiwamo za mahusiano," amesema Dendego.

Mkuu huyo wa Mkoa ameongeza kuwa maadili ya walimu na wanafunzi ni jukumu la wakuu wa shule kwani hivi sasa misingi ile ya zamani imeachwa hali ambayo imesababisha watoto kutokuwa na maadili mazuri.

"Tumeacha tamaduni tulizolelewa tunaacha wanafunzi wafanye wanavyotaka,tunawapa muda mwingi wa kupumzika,mbaya zaidi mwanafunzi anafanya kasa halafu anabembelezwa sasa hapo ufaulu utatoka wapi,"amesema Dendego.

Amesema wakati umefika kwa walimu kujitahidi kurejesha utamaduni wa kuwajenga watoto wawe katika maadili mazuri na kuzingatia masomo.

"Inashangaza hivi sasa mhitimu anakuwa hata hawezi kujieleza kuomba kazi ni kwasababu msingi wa elimu haujajengwa, mimi hapa nilichapwa wakati nasoma na hivi sasa ni  Mkuu wa Mkoa," amesema.

Dendego amesema wakati sasa umefika wa shule kurudishwa ziwe chuo cha mafunzo na hivyo kuondoa tatizo la sasa la watoto kushinda kwenye mitandao ya kijamii ambayo haiwasaidii kielimu.

Naye Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Dk.Elipidius Baganda, amesema hali ya kitaalam kwenye mkoa huo kwa mwaka jana mitihani yote ya taifa ukiondoa wa darasa la nne ufaulu umeongezeka ukilinganisha na ilivyokuwa huko nyuma.


Dk.Baganda amesema mkoa unaendelea kujipanga ili kuongeza ufaulu zaidi ambapo katika mkutano wa Maafisa Elimu wa Mikoa uliofanyika hivi karibuni mkoani Mbeya mikoa ya Singida,Dodoma sasa itakuwa inashindanishwa na Iringa,Dar es Salaam na Tanga kwenye mitihani.


MWISHO

«
Next
Newer Post
»
Previous
Older Post

No comments:

Leave a Reply