WAKULIMA SINGIDA WAKUBALI KILIMO IKOLOJIA

 




Na Amini Nyaungo

 

Kilimo ndio uti wa mgongo asilimia  tisini ya Wananchi wa Tanzania maisha yao wanategemea kilimo, tena kilimo cha chakula kwa ajili ya familia zao huku kila kaya ikihesabiwa inakula gunia moja kwa mtu mmoja hivyo kutokana na ukubwa wa familia ndio jitihada zinafanyika na wakulima wasipatwe na baa la njaa.

 

 

Tanzania ina aina nyingi ya kilimo kwa wanaojishughulisha na kilimo, hii inatokana na ubora wa ardhi na maeneo waliyopo,huku kilimo cha Ikolojia kwa mkoa wa Singida kinaonekana kupendwa zaidi baada ya kupata elimu hiyo kutoka katika kituo cha Standard Radio kilichopo mkoani hapa na Maafisa kilimo. 

 

KILIMO CHA IKOLOJIA NI NINI ?

 

Hiki ni kilimo kinachofuata utaratibu bora wa kilimo ambapo hakitumii kemikali katika mazao yake huku kikifuata kanuni bora za kilimo ambazo hauathiri udongo pamoja na kulinda ardhi. 

 

Baada ya kupata elimu hiyo ya kilimo cha kiikolojia wakulima mbalimbali kutoka mkoani Singida wameelezea namna walivyokipokea kilimo hiko.

 

Mkulima Madai Njou kutoka kijiji cha Unyangwe Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi yeye amesema kuwa amenufaika na kilimo hiko kwa mambo yafuatayo.

 

Shamba lake halijapoteza rutuba yake baaada ya msimu kuisha kwani hachomi masalia ya mazao bali anayaacha yaoze na baadae kupata mbolea.

 

Lakini pia anahifadhi mbegu kwa kutumia ghala ambapo hazibunguliwi na  wadudu na msimu wa kilimo ukifika anazitoa na kupanda.

 

" Mimi nimenufaika na kilimo cha Kiikolojia kwani shamba langu linapata rutuba kwa kufuata kanuni za kilimo hiki moja ya kanuni hizo ni kutochoma masalia ya mazao , lakini pia hata uhifadhi wangu wa mbegu nahifadhi kwa njia za asili ambazo ni bora sana hazitumii madawa," Njou.

 

Rehema Joel Mbula yeye mkazi wa Ilongero mkoani hapa anasema kuwa katika shamba lake anatumia mbolea za asili ambazo zinaendana na kilimo cha kiikolojia mbolea ambazo hazitumii kemikali hivyo hata mazao yake yanakuwa salama.

 

Ameelezea kuwa anatumia Bangi ya Mbwa, Mabilingali hata majani ya miti kwa ajili ya kutengeneza viwatilifu kwa ajili ya kuua wadudu.

 

Akisema kuwa zile mbolea za kuuzwa zina kemikali anaamini kuwa zikitumika katika vyakula mfano mbogamboga zinaweza kuleta madhara kwa mtumiaji

 

" Mimi nafarijika sana kukifahamu kilimo cha Kiikolojia kwani kimenifanya nitumie mbolea za asili ambazo natengeneza mwenyewe kwa ajili ya kuua wadudu wakorofi lakini mbolea ya mavi ya Ng'ombe ni mbolea nzuri sana nitumia sana, '' Mbula.

 

Naye Zaina Nkungu kutoka kata ya Msisi akiweka wazi kuwa hakuna kilimo bora na rahisi kama Kiikolojia kwani unaweza ukafanya kilimo mseto na ukafanikiwa kupata mazao mengi kwa msimu mmoja.

 

"Elimu ya Kiikolojia imetusaidia na tunaitekeleza kwani hadi sasa sisi watu wa Msisi tunaitekeleza hiyo kwa vitendo na tunalima kilimo mseto katika mashamba yetu.

 

Baada ya maoni ya wakulima juu ya kulimo cha Ikolojia nikafanya jitihada kumtafuta Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Singida Salumu Athuman atueleze baadhi ya maoni ya wakulima juu ya kilimo cha Kiikolojia na vipi utekelezaji wake  ukoje ikiwa yeye ndio msimamizi mkuu ?

 

Afisa kilimo Salum Athumani ameeleza kuwa wakulima wanakifuatilia kwa karibu kilimo hiko na kila mkulima anakitekeleza kwa eneo analoliongoza kwani wanaona ni kilimo rafiki kwao.

 

"Wanatekeleza kilimo cha kiikolojia kwa ukubwa wake kwani wao wanaona ni kilimo rahisi na kinachojifadhi mazingira," Salum.

 

Juu ya kilimo mseto Salum Athumani amesema kuwa yeye kama Afisa Kilimo anajitahidi kuwaelekeza juu ya kilimo mseto ambacho pia kinafanywa na aina hii ya Kilimo cha Ikolojia.

 

Licha ya kuwaeleza hayo bado ameendelea kuwakumbusha kuwa kila familia ihesabu watu wake kwani kila mtu anauwezo wa kula gunia moja la mahindi kwa mwaka hivyo wajitahidi kulima kwa kufuata utaratibu ili wapate manufaa.

 

“ Mtu mmoja anakula gunia moja la mahindi kwa mwaka hivyo familia ihesabu ina watu wangapi wahifadhi chakula baada ya mavuno,” Salumu

 

Kwa upande wa Afisa kilimo wa Halmashauri ya Ikungi Boniface Barnaba yeye amebainisha kuwa kilimo cha Ikolojia kina maana kubwa kwa Watanzania kwani kilimo hiki kikiendelezwa kinaweza kusaidia kuondoa baa la njaa kwa familia kwani ni kilimo rahisi kinacholeta mazao mengi.

 

“ Hiki kilimo ni muhimu sana sisi maafisa kilimo tunafanyakazi kubwa kuwaelemisha lakini pia tunawashukuru Standard Radio kwa kutoa elimu hii kwani wakikizingatia kilimo hiki wanaweza wakajikomboa katika baa la njaa ambalo kwa msimu chakula huwa hakikutani na kile cha msimu unaofuata,” Boniface

 

Baada ya kusikia hayo yote nimejaribu kumtafuta daktari kutoka hospitali ya Mandewa mkoani Singida Daktari Mtani na nikamuuliza juu ya binadamu kutumia  vyakula vyenye viwatilifu vilivyowekwa sumu inaathiri vipi katika maisha yake.

 

Amesema kuwa kuna magonjwa mengi yanaweza kutokea kwa kutumia vyakula ambavyo vimepulizia kemikali wakati vipo shambani.

 

 

Mtani amesema kuwa ile kemikali inamadhara yake yanaweza yakakupata taratibu na madhara yake huenda yakatokea miaka mingi baadae.

 

“ Siku hizi mashambani wnapulizia sumu kuua wadudu wakati mwingine zile mboga zinashika ile sumu na inaathiri moja kwa moja mtumiaji hivyo ni kweli,” Mtani

 

Mkoa wa Singida ni moja ya mikoa ambayo ina wakulima wengi na shughuli kubwa ni kilimo na  Alizeti ni zao linaloitambulisha vyema Singida lakini wakulima wa eneo hili  wanalima mazao mbalimbali.

 

Moja ya mazao wanayolima ni pamoja na Mahindi, Mtama aina ya Rangi ranga, wele, ulezi, Kitunguu, Viazi vitamu, Viazi lishe pamoja na Dengu.

 

Katika kila zao lina muda wake huku  kwa mujibu wa Afisa kilimo Salum Athumani anasema kuwa kuna baadhi ya mazao hayahitaji mvua nyingi kama vile Dengu hivyo mara zote linalimwa baada ya kuvana au inapokaribia kuvana zile mvua za mwisho mwisho ndio zoa hili linalimwa.

 

Kwa mazao mengine inatoka na msimu wa mvua ulivyo basi unaweza kulima na kupanda na ukafanikiwa katika kilimo chako.

 

Msimu wa kilimo mkoani Singida ni kuanzia mwezi wa kumi na moja kwenda mwezi wa kumi na mbili ambapo hapo ndio mvua za awali zinaanza lakini matayarisho ya shamba yanaanzia mwezi wa kumi na moja.

 

Endapo wewe mkulima au mgeni katika eneo hili ukitaka kulima kuna wakazi ambao wanakodisha mashamba yao kwa msimu mmoja ambapo ekari moja elfu thelathini (30,000) au Elfu Hamsini (50,000) viwango vya bei vinatokana  na ardhi ambapo kuna aina mbili ya ardhi mbuga na kichanga.

 

Hiyo ndio Singida iliyopo katikati mwa Tanzania na utaratibu wao baada ya kilimo wakati wa mavuno wakazi wa huku wanafanya starehe mbalimbali kwa ajili ya kujipongeza baada ya kazi ya muda mrefu.

 

Mwisho


Post a Comment

Previous Post Next Post