Na Mwandishi Wetu ,Arusha
Katibu wa Bunge la Tanzania, Baraka Leonard, amesema Tanzania iko tayari kujifunza kutoka mabunge ya nchi nyingine na pia kushirikisha uzoefu wake katika uendeshaji wa Bunge.
Akizungumza Arusha wakati wa mkutano wa makatibu wa mabunge unaofanyika sambamba na Mkutano wa 153 wa Inter-Parliamentary Union (IPU), amesema hakuna mfumo mmoja wa Bunge unaoweza kusemwa kuwa bora kwa kila nchi.
Amesema Tanzania ina Bunge la chombo kimoja, tofauti na baadhi ya nchi zenye mabunge mawili, hivyo kubadilishana uzoefu kunasaidia kujifunza njia bora za kuendesha shughuli za kibunge.
Leonard pia amesema Tanzania imeendelea kutumia teknolojia kupitia mfumo wa e-Parliament, unaowawezesha wabunge kupata nyaraka mtandaoni na kupunguza matumizi ya karatasi.
Aidha, amesema Bunge limeongeza uwazi kwa wananchi kupitia televisheni ya Bunge na mitandao ya kijamii, ambapo wananchi wanaweza kufuatilia mijadala na shughuli za Bunge.
Mkutano huo unaendelea Arusha, ukiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu kati ya mabunge mbalimbali duniani.
Mwisho


Post a Comment