Na Thobias Mwanakatwe
PUNDA wawili wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo kasi katika barabara kuu ya Arusha–Namanga, eneo la Engikaret, Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, huku mizoga yao ikiachwa kando ya barabara kwa zaidi ya nusu siku bila kuondolewa.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 16, mwaka huu, ambapo kwa mujibu wa mashuhuda, punda hao waligongwa na gari hilo usiku wa manane au alfajiri, kabla ya dereva kuondoka eneo la tukio.
Mbarwa Kivuyo, kutoka taasisi ya Kangai Foundation na mwanachama wa Chama cha Kitaifa cha INADES FTZ, alisema alishuhudia tukio hilo alipokuwa akisafiri kutoka Arusha kwenda Longido kuhudhuria kikao cha Kamati ya Wilaya ya Usimamizi wa Biashara ya Hewa Ukaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido.
Alisema kilichomsikitisha zaidi ni kukuta mizoga ya punda hao ikiwa bado kando ya barabara saa 8:00 mchana alipokuwa akirejea Arusha, hali iliyoibua maswali kuhusu hatua zilizochukuliwa na mamlaka husika kufuatia ajali hiyo.
Kivuyo alisema alitamani kusimama eneo la tukio ili kufahamu kama gari lililowagonga punda hao lilikuwa limetambuliwa na kama dereva wake alikuwa amechukuliwa hatua, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na majukumu mengine rasmi aliyokuwa nayo.
Alisema tukio hilo linaashiria changamoto ya kutokuwapo kwa uwajibikaji wa baadhi ya madereva wanaogonga mifugo na kuondoka bila kutoa taarifa, huku wanyama hao wakiwa na umuhimu mkubwa kwa maisha na uchumi wa jamii zinazotegemea ufugaji.
Alieleza kuwa punda ni muhimu kwa familia nyingi katika wilaya za Longido, Simanjiro na Monduli, kwani hutumika kusafirisha mizigo, kuchota maji na kusaidia shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazoiwezesha jamii kujipatia kipato.
Kutokana na hali hiyo, Kivuyo ameiomba taasisi ya Brooke East Africa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Longido pamoja na Jeshi la Polisi kuimarisha usimamizi wa sheria na kuhakikisha madereva wanaosababisha vifo vya mifugo wanachunguzwa na kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Aidha, amependekeza kuwekwa kwa alama za barabarani zinazoonyesha maeneo ya wanyama kuvuka, matuta ya kupunguza mwendo na kuimarishwa kwa usimamizi wa viwango vya mwendo wa magari katika maeneo yanayokumbwa na ajali za mifugo.
Alisisitiza umuhimu wa kutoa elimu kwa madereva, hususan wanaotumia barabara ya Arusha–Namanga, wakiwemo madereva wa malori yanayovuka mipaka ya nchi, kuhusu wajibu wao wa kuzingatia usalama wa barabarani na kulinda mifugo.
Pia, alihimiza kuimarishwa kwa mifumo ya kuripoti matukio ya ukatili dhidi ya wanyama kwa kuwashirikisha wamiliki wa punda na wahudumu wa afya ya wanyama katika jamii ili kuhakikisha matukio kama hayo yanaripotiwa kwa wakati na kufanyiwa uchunguzi.
Alisema vifo vya punda hao havipaswi kuchukuliwa kama jambo la kawaida, akisisitiza kuwa kulinda ustawi wa wanyama ni sehemu ya kulinda maisha na uchumi wa jamii zinazowategemea.
“Haki kwa punda wa Engikaret ni haki kwa punda wote nchini Tanzania,” alisema Kivuyo.
MWISHO

Post a Comment