Na Jumbe Ismailly MANYONI
MBUNGE wa jimbo la Itigi,lililopo Halmashauri ya Itigi, wilayani Manyoni,Mkoani Singida,Yohana Stephen Msita ni mbunge wa kwanza tangu nchi ilipopata uhuru wake 1961 kufika katika Kitongoji cha Kipera,Kijiji cha Ipalalyu,Kata ya Mitundu,wilayani Manyoni.
Kauli hiyo ilitolewa na kiongozi wa wafugaji wa jamii ya kabila la wasukuma wanaoishi katika maeneo hayo,Omari Bakari Makanja,maarufu kwa jina la Mwananyiinzi,kwenye mkutano wa mbunge huyo na wafugaji wa Kijiji cha Kipera uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Kipera.
“Karibu sana Mbunge,karibu diwani na msafara wako mliofuatana ninashukuru sana Kata ya Mitundu haijawahi kutokea mbunge kama huyo kututembelea mpaka huku,ninashukuru sana………………………….
Jamani mimi tangu nihamie Mitundu hii haijawahi kutokea diwani kama huyu waongozane na wabunge na msafara wote wa viongozi kutoka wilayani mpaka huku maporini, jamani watu wa Kipera ni jambo la kushangaza sana mbunge kama huyu ana moyo gani”alisisitiza huku akionesha mshangao.
Hata hivyo kiongozi huyo wa wafugaji aliweka bayana pia kwamba kabla ya kuwasilisha kilio chao walichomuitia hadi kufika huko,watu wa Kipera wachungaji tunapenda kumpa pongezi mbunge wetu kwa kumkabidhi shilingi 30,000/= iwapo atahitaji kuongeza mafuta ya gari lake asiweze kutumia fedha zake,kutokana na shukurani aliyowafanyia wananchi wa maeneo hayo.
Kupitia kikao hicho cha kuwasikiliza kero zao wafugaji wakaahidi pia kwamba endapo Mbunge huyo ataendelea kuwa na moyo wa aina hiyo wa kuwatembelea wafugaji mara kwa mara na kuwasaidia kuwatatulia kero zao, wakaahidi kumkabidhi zawadi ya ng’ombe.
“Kama mbunge akiendelea kututembelea mara kwa mara na kututatulia kero zetu tunazolia hapa wafugaji na wananchi kwa ujumla,kuna ng;ombe wake tutakuja kumwambia mheshimiwa mbunge njoo na kenta ya kubebea ng;ombe aliyenona”alisisitiza huku akishangiliwa na wafugaji pamoja na wananchi kwa ujumla waliohudhuria mkutano huo.
Naye Mbunge wa jimbo la Itigi,Yohana Stephen Msita baada ya kauli ya wafugaji hao alisisitiza kwamba pamoja na watangulizi wake kutofika kwenye Kitongoji na Kijiji hicho kwa ujumla kwa upande wake atakuwa akiwatembelea mara kwa mara mpaka watamchoka wao wenyewe.
“Na hapa Kipera ntakuja sana umenigusa sana uliponiambia eti mbunge hajawahi kuja hapa nikajisikia vibaya sana,mimi niliwaambia siyo mbunge wa mjini mimi kwetu ni pale kijiji cha Doroto,kwa hiyo mimi ni mwanakijiji mwenzenu”alifafanua mbunge huyo.
“Nitakapopanga ziara ya jimbo zima na Kipera nitakuja tena,tuje tucheze ngoma za akisukuma kweli kweli sasa nikija hapa mniandalie fimbo nzuri na kaniki tuje tufurahi pamoja”alisisitiza Msita huku akishangiliwa na wananchi.
Post a Comment