Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mbunge wa Iramba Mashariki, Jesca David Kishoa, ameomba mwongozo Bungeni kufuatia kutoridhishwa na majibu ya Serikali kuhusu ujenzi wa soko la mazao katika Wilaya ya Mkalama.
Mbunge huyo amesema hatua hiyo imekuja baada ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Festo Dugange, kueleza kuwa maafisa wa Serikali wapo eneo la mradi wakifuatilia utekelezaji, jambo ambalo alidai halina uhalisia.
Kishoa ameliambia Bunge kuwa ofisi yake imefanya ufuatiliaji wa haraka kwa kuwatuma maafisa wake eneo husika, ambapo walifika katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi pamoja na Idara ya Mipango, lakini taarifa walizopata zinaonesha kuwa afisa wa mwisho wa Serikali alionekana katika eneo hilo Septemba 9, 2024.
“Tunapokuwa hapa ndani tuna access na majimbo yetu na tunajua nini kinaendelea. Unapopewa majibu ambayo hayaridhishi linatuumiza sana,” amesema Kishoa.
Kutokana na hali hiyo, ameomba mwongozo wa Mwenyekiti wa kikao kuhusu hatua za kuchukua dhidi ya majibu aliyoyaita kutokuwa sahihi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa kikao cha Bunge, Najma Murtaza Giga, amesema watarudi kwenye kumbukumbu rasmi za Bunge ili kujiridhisha na ukweli wa majibu yaliyotolewa kabla ya kutoa uamuzi.

Post a Comment