Na Baraka Nzobo
Mashine za X-ray za Kinywa na Meno ni nyenzo muhimu zinazo muwezesha Daktari wa Kinywa na Meno kugundua matatizo yaliyojificha ndani ya jino, maambukizi kwenye mfupa wa taya , mifupa mingine ya uso, vimbe na saratani za Kinywa na Meno matatizo ambayo ni vigumu kugundulika kwa uchunguzi wa kawaida wa kimatibabu. Mashine hizi humuwezesha Daktari wa Kinywa na Meno kungudua matatizo yaliyojificha ya Magonjwa ya Kinywa na Meno na pia humuwezesha Daktari kupanga matibabu sahihi ya Magonjwa ya Kinywa na Meno. Kuna aina kuu tatu za mashine za X-ray za Kinywa na Meno ambazo zinatumika ndani ya nchi ya Tanzania, mashine hizo ni:
1. Mashine ya Kidijitali ya Kiradiolojia ya meno (Digital Periapical Dental X-ray): Mashine hii hupiga picha ya jino kuanzia sehemu ya kutafunia hadi kwenye mzizi.
2. Mashine ya Kidijitali ya kiradiolojia ya Kinywa kizima (2D- Orthopantomography (2D-OPG): Mashine hii hupiga picha ya Kinywa kizima na kuonesha meno yote pamoja na taya na matundu yote eneo la Kinywa na Meno.
:
3. Mashine ya CT-Scan ya Kinywa na Meno (3D-Cone Beam Computed Tomography (3D-CBCT): Mashine hii hupiga CT-scan ya magonjwa ya Kinywa na Meno, OPG na vipimo vingine vingi eneo la Kinywa.
Kwa muda mrefu imezoeleka mtu kwenda kiliniki ya Kinywa na Meno na kufanyiwa matibabu ya jino (Kuziba au Kung’oa) bila mgonjwa kupigwa X-Ray ya jino kujua ukubwa wa tatizo na aina gani ya matibabu inayofaa kufanyika kwenye jino husika. Jambo hili limekuwa likileta madhara mbalimbali kwa wagonjwa kama vile:
1. Mgonjwa kung’olewa jino ambalo siyo bovu (linang’olewa jino zima linaachwa jino bovu)
2. Mgonjwa kuzibwa jino kwa aina ya uzibaji ambao sio wenyewe. Jino bovu likipigwa X-ray itamuonyesha Daktari wa Kinywa na Meno aina sahihi ya matibabu ya kuziba yanayotakiwa kufanyika. Ukitaka kufanya matibabu ya mzizi au kiini cha jino ni lazima uongozwe na X-ray ya jino mpaka matibabu yatakapokamilika.
3. Mgonjwa kucheleweshwa kugundulika tatizo linalomsumbua mapema eneo la Kinywa hivyo kumletea madhara makubwa ya kiafya.
Wito:
Wizara ya Afya inazikumbusha Hospitali zote, vituo vya Afya Pamoja na Kliniki za SERIKALI na BINAFSI zinazotoa Matibabu ya Kinywa na Meno kuhakikisha zinanunua na Kufunga Mashine za X-ray za Kinywa na Meno kulingana na miongozo iliyotolewa na Serikali ili wananchi wapate huduma iliyobora ya matibabu haya. Wizara inawahimiza Wananchi kudai haki ya kupigwa picha za X-ray za Meno na kuoneshwa uharibifu uliopo kwenye Jino au Meno husika na kuambiwa aina sahihi ya matibabu yanayopaswa kufanyika.



Post a Comment