MSONGO WA MAWAZO HULETA VIDONDA MDOMONI VYENYE MAUMIVU MAKALI

 Na Dokta Baraka Nzobo



Inawezekana katika maisha yako umeshawahi kupata vidonda vidogo kwenye ulimi, fizi au shavu la ndani mdomoni ambayo vina maumivu  makali na maumivu hayo huongezeka  pindi ulapo vitu vyenye chumvi (kama vile mchuzi, supu), viungo vingi, au vyakula vyenye uchachu wa tindikali kama (limao, chungwa na chenza). Vidonda hivi ambayo inawezekana umeshawahi kuvipata huwa vinasababishwa na tatizo la Msongo wa Mawazo (Mental Stress) ambao mtu anakuwa ameupitia au anaupitia kutokana na sababu mbalimbali. Vidonda hivi mdomoni kwasababu ya Msongo wa Mawazo (stress) hupona vyenyewe ndani ya wiki moja au mbili toka kutokea kwake. Hali ya kuwa na hofu pia huchangia kuleta vidonda mdomoni vyenye maumivu makali.

*Uhusiano wa Msongo wa Mawazo na kupata vidonda mdomoni vyenye Maumivu makali*



1. Msongo wa Mawazo (Stress) husababisha kushuka kwa kinga ya mwili inayosaidia kupambana na maambukizi madogo (minor infections) mwilini hivyo kukiweka Kinywa kwenye hatari ya kupata vidonda.

2. Msongo wa Mawazo (stress) hufanya mtu kutafuna meno yake mwenyewe bila kujitambua au kujitafuna maashavu yake ya ndani bila kujitambua.

3. Msongo wa Mawazo (stress) husababisha kupungua kwa kiwango kikubwa cha uzalishaji wa mate mdomoni hali inayofanya mdomo kuwa mkavu na hivyo kushindwa kupata ulinzi wa kupambana na maambukizi unaotolewa na uwepo wa mate mdomoni. Mate yana kemikali zinazosaidia kupambana na maambukizi ya Bakteria mdomoni.

4. Msongo wa Mawazo (stress) husababisha mtu kusahau kupigwa Mswaki Meno yake na usafi mwingine wa Kinywa hivyo kusababisha kuwa na Kinywa kichafu hali inayoongeza hatari ya kupata maambukizi mdomoni.


*Makundi ya watu wanaoathirika zaidi*


Watu wa jinsia na rika lote huathirika na changamoto hii ya vidonda mdomoni  (Mouth Ulcers) vyenye maumivu kwa sababu ya msongo wa Mawazo. Makundi ambayo mara kwa mara yamekuwa yakienda Hospitali kupata matibabu kutokana na changamoto hii:

1. Wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo wanapokaribia kufanya mitihani. Hofu ya kufanya mtihani na kuwaza namna matokeo ya mtihani huo yatakavyotoka huchangia sana wanafunzi kupata vidonda hivyo.

2. Wafanyakazi ambao hufanya kazi katika ofisi ambazo mazingira ya kazi husika humfanya mfanyakazi kushindwa kuhimili matarajio ya ofisi hivyo kumfanya kupata msongo wa Mawazo (stress)

3. Wanandoa waliopeana talaka au Wapenzi walioachana: Katika wanandoa waliopeana talaka, kuna mwanandoa mmoja hupitia msongo mkali wa Mawazo (stress) ambao humpelekea kupata vidonda hivyo. Hali hii pia huwapata wapenzi waliochana kwenye mahusiano yao ya kimapenzi, mpenzi mmoja huathirika na hali hii.

4. Ugumu wa maisha: Ugumu wa maisha hupelekea baadhi ya watu kupata msongo wa Mawazo (stress) na kufanya mtu huyo kupata vidonda hivyo mara kwa mara.

*Matibabu na Kinga*

1. Punguza msongo wa Mawazo kwa kufanya shughuli mbali zitakazo kusaidia kuondokana na Mawazo na pia upate muda mzuri wa kulala usingizi. Epuka mazingira yote yanayoweza kukuletea msongo wa Mawazo (stress)

2. Epuka kula vyakula vyenye chumvi (Supu au Mchuzi), viungo vingi au vyakula vyenye uchachu wa tindikali kama vile machungwa, limao au chenza

3. Tumia mswaki wenye brush laini kupigia mswaki meno yake ili usiweze kujitonesha kwenye vidonda au kidonda kilichotokea.

4. Nenda Hospitali kamuone Daktari wa Kinywa na Meno ili aweze kukuchunguza na kukupatia dawa maalumu za kuondoa maumivu makali unayoyapata.


*BY DR BARAKA J NZOBO*

Post a Comment

Previous Post Next Post