Na Dokta Baraka Nzobo
Kama wewe ni mtumiaji wa Dawa za Meno zenye madini ya Fluoride utakuwa umeona msimbo wa rangi (colour code) chini ya chupa au mirija ya plastiki ya dawa yako ya meno. Rangi hizo ni Nyekundu, Kijani, Bluu au Nyeusi. Rangi zinazopatikana chini ya mirija ya dawa za meno (kijani, bluu, nyekundu, au nyeusi) ni alama za utengenezaji tu (color marks or eye sensor) zinazotumiwa na mashine kukata na kufunga mrija, hazionyeshi viambato vya dawa hiyo. Rangi hizo hazina uhusiano na usalama au viambato vya dawa unayoitumia. Kagua hata chupa za maji ya kunywa toka viwandani angalia karatasi la nailoni lililozungushiwa kwenye chupa hiyo utaona msimbo wa rangi nyeusi, nyeupe hata kijivu kulingana na uchaguzi wa kiwanda kinachotengeneza maji hayo ya Kunywa.
*Kwa ufupi:*
1. Kijani, Bluu, Nyekundu, Nyeusi: Zote zina lengo moja la kiufundi la kiwanda (eye sensor) inayoiambia mashine hapa ndipo mwisho wa mrija au chupa, kata na funga mrija huo baada ya dawa kujaa.
2. Taarifa za Viambato: Kusoma orodha ya viambato vilivyomo kwenye dawa ya meno angalia sehemu iliyoandikwa *("Ingredients")* ndiyo njia pekee ya kujua kilichomo.
3. Usalama: Rangi hizo hazimaanishi kama dawa ni ya asili (mitishamba), au imechanganywa na dawa, au kemikali.
*Ushauri:*
Tunaishauri jamii nzima ya Watanzania kuepuka kutoa maneno ya upotoshaji kwa watu ambao hawawezi kutafuta ukweli wa jambo linalozungumzwa. Lakini pia tunawashauri watanzania wajenge mazoea ya kutafuta ukweli wa kisayansi kutoka kwa wataalamu wa eneo husika ambalo upotoshwaji huu unafanyika. Madaktari wa Kinywa na Meno wapo nchi nzima waulizwe maswali yote pindi pale inapotokea mtu huelewi jambo kwa usahihi.
*By: DR NZOBO*


Post a Comment