MWANGI: MKINICHAGUA NITAHAKIKISHA TAA ZA BARABARA ZINAWEKWA MITAANI

 

Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 



MGOMBEA udiwani katika Kata ya Ipembe Manispaa ya Singida kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Omari Mwangi, amezindua kampeni zake huku akielezea vipaumbele vyake ikiwa wananchi watampa ridhaa ya kuwa diwani.


Akizungumza na wananchi katika mtaa wa Jamatini leo (Septemba 5,2025) amesema moja ya vipaumbele vyake iwapo wananchi watamchagua ni kuhakikisha taa zinawekwa katika barabara zilizopo katika  kata hiyo ili wajasiliamali waweze kufanya biashara zao masaa 24 na hivyo kuinua uchumi wao.



Mwangi amesema kipaumbele kingine akichaguliwa ni kuhakikisha vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vilivyosajiliwa vilivyopo katika kata hiyo vinapata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Manispaa ya Singida.


Jambo jingine atakalolifanya ni kuinua selta ya michezo hasa ikizingatia kuwa kata ya Ipembe ndio kioo cha Manispaa ya Singida hivyo inatakiwa mambo makubwayafanyike hapo na kisha kata nyingine ziweze kujifunza.



Mwangi akizungumza suala la wafanyabiashara wadogo maarufu wamachinga, amesema ujenzi wa barabara utakapoanza atahakikisha anashawishi madiwani wenzake ndani ya Baraza la Madiwani wa Manispaa ili wamachinga wahamishiwe katika stendi ya zamani ya mabasi kuendelea na biashara zao kupisha ujenzi wa barabara.



Aidha, Mwangi amesema uongozi wake utakuwa ni shirikishi ambapo mipango yote ya maendeleo katika kata hiyo atafanya mikutano ya wananchi kuwashirikisha pamoja na kushikiliza kero zinazowakabili ili zile ambazo zipo ndani ya uwezo wake aweze kuzitatua hapo hapo na zile ambazo zitahitaji kuziwasilisha serikalini atafanya hivyo.


Amewaomba wananchi Oktoba 29, 2025 wasifanye kosa wahakikishe wanampigia kura mgombea urais kupitia CCM Dk.Samia Suluhu Hassan, mgombea ubunge Singuda mjini, Yagi Kiarati na yeye mgombea udiwani kata ya Ipembe Omari Mwangi.



Awali Mwenyekiti wa Tawi namba moja CCM mtaa wa Jamtini, Nestory Massawe,amesema kilio kikubwa cha wafanyabiashara wadogo ni sehemu ya kufanyia biashara zao ujenzi wa barabara utakapoanza na kumuomba mgombea huyo alitilie uzito suala hilo.

Post a Comment

Previous Post Next Post