MWAKAJUMBA ATOA NENO KWA WAGOMBEA WALIOTEULIWA KUWANIA UDIWANI

 

Na Thobias Mwanakatwe, KYELA



MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa kutoka Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, Paul Mwakajumba,amewaomba wagombea waliopata nafasi ya kuteuliwa kuwania udiwani kuhakikisha wanaweka mikakati ya kukifanya chama kinapata ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.


"Pamoja na salamu napenda kutumia nafasi hii adhimu kuwapongeza wateule wote kwa nafasi ya udiwani nchi nzima ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hasa katika Wilaya yetu pendwa na Jimbo letu la uchaguzi la Kyela lililopo Mkoa wa Mbeya," alisema Mwakajumba.


Mwakajumba alisema walioteuliwa kugombea udiwani watambue kuwa huu siyo muda wa kushangilia kwa kuteuliwa  na kuaminiwa na chama kupeperusha bendera ya CCM bali ni muda wa kutafakari kazi kubwa na majukumu mazito yaliyo mbele yao kwanza kutafuta kura za kishindo kwa CCM  ngazi ya Rais, Mbunge na Diwani.


"Pia huu ni muda wa  kuandaa mpango kazi wako wa namna utakavyoenda kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia ahadi zako wakati wa kampeni na ilani ya CCM 2025 - 2030,tukumbuke kwa pamoja tutashinda, umoja wetu ndiyo ushindi wetu kwa Chama Cha Mapinduzi," alisema.


Aidha, Mwakajumba aliomba  makundi yote yazikwe maana hivi sasa tunakipigania Chama Cha Mapinduzi ili tupate ushindi wa kishindo kwa CCM. 


"Tayari tuna mteule wetu kwa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Mungano wa Tanzania, ambaye ni Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza ni Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, kule Zanzibar tunaye Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ila kwa nafasi ya Ubunge bado tunasubilia nani atateuliwa ila kwa Udiwani ni wewe Diwani Mteule," alisema.


"Hongera sana na ninakupongeza hivyo basi wakati ukifika wa kampeni , twendeni kwa wananchi kama CCM na siyo MTU maana hakuna aliye juu ya Chama Cha Mapinduzi na Mungu wa mbinguni awabariki sana," alisema Mwakajumba.

Post a Comment

Previous Post Next Post