OFISI YA MWANASHERIA MKUU YAWAALIKA WANANCHI KUPATA HUDUMA ZA KISHERIA

 

Na Thobias Mwanakatwe, DODOMA 



OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imewaalika wananchi kufika katika banda lake  kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma ili waweze kutatuliwa migogoro na malalamiko yanayowakabili yanayohusu masuala ya kisheria. 


Wakili wa Serikali Mkuu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jackson Nghoboko akizungumza leo (Juni 19, 2025) amesema ofisi hiyo imeweka kambi kwenye viwanja hivyo ili  kutoa elimu na ushauri wa Kisheria pamoja na kutatua migogoro na malalamiko yanayowakabili wananchi. 


“Tunaendelea kutoa elimu na ushauri wa kisheria kwa wananachi wanaokuja hapa, pia migogoro inayohusu masuala ya Ardhi, ndoa na masuala ya ya matunzo ya watoto tumekuwa tukiipokea na kuishughulikia,” amesema Nghobolo 



Aidha,  Nghoboko ametoa wito kwa wananchi wa Jiji la Dodoma kuendelea kujitokeza kwa wingi katika banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupata ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za Kisheria zinazowakabili.

“Nitoe rai kwa wananchi wa Dodoma waje kwenye banda letu lililoko katika maadhimisho haya ya Utumishi wa Umma hapa Chinangali tuwahudumie, huduma zote tunazozitoa hapa ni bure kabisa.” amesema Nghoboko.

Kwa upande wake mmoja ya wananchi waliotembelea banda la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi Magreth Kapele amefurahishwa na huduma zinazotolewa na Mawakili wa Serikali katika banda hilo, ikiwemo ushauri wa kisheria unaotolewa.

 


“Nimefika kwenye banda hili la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nimehudumiwa vizuri, maswali mengi ambayo yalikuwa yananitatiza nimejibiwa kwa ufasaha kwakweli nimejifunza mambo mengi,” amesema Magreth  


Naye, Bw. Eduard Sunday, ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutoa huduma bora kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kulipia huduma za kisheria, pia ameipongeza Ofisi hiyo kwa kutoa huduma kwa haraka na kwa urahisi.


“Naishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutupatia huduma kisheria bure na kwa haraka, nimefika hapa nimehudumiwa vizuri na Mawakili nawapongeza sana,” amesema Sunday.



Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma yameanza 16 Juni 2025 na yatahitimishwa 23 Juni, 2025, ambapo Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kutoa huduma za Ushauri wa Kisheria, Elimu ya Sheria, Utatuzi wa Migogoro na kushughulikia malalamiko ya wananchi.

Post a Comment

Previous Post Next Post