SHUGHULI ZA UTALII ZAINGIZIA SERIKALI BILIONI 12.65

Na Jumbe Ismailly MANYONI

 


SERIKALI kupitia Wakala wa Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya kati imefanikiwa kuingiza takribani shilingi bilioni 12,657,626,387.60 kutokana na shughuli za utalii zinazofanyika katika mapori ya Akiba ya Rungwa-Kizigo na Muhesi.

 

Kamanda wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Kanda ya kati,Kamishna Msaidizi Mwandamizi,Herman Nyanda amebainisha hayo alipokuwa akielezea faida zitokanazo na utalii na kwamba kiasi hicho cha fedha kimepatikana katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2022/2023,2023/2024 na 2024/2025.

 


Aidha Kamanda huyo wa Tawa Kanda ya kati amefafanua kuwa utalii wa uwindaji unahusisha seehemu kubwa ya kanda ya kati-Manyoni Mkoani Singida na unafanyika katika Mapori ya Akiba matatu ambayo ni pamoja na Rungwa,Kizigo na Muhesi na eneo la nje la Rungwa-North lililopo Halmashauri ya Itigi.

 

Kwa mujibu wa Kamishna Nyanda mapori hayo kwa pamoja yana jumla ya vitalu 12 ambapo pori la Akiba Rungwa lina vitalu sita,Kizigo vitalu vinne,Muhesi kitalu kimoja na Rungwa North Open Area kitalu kimoja na kwamba kati ya vitalu 12 vilivyopo,vitalu tisa vimepata wawekezaji wa utalii wa uwindaji.

 

Akifafanua zaidi kamishina huyo amesema wawekezaji hao wamekuwa wakifanya kazi za uhifadhi,kuboresha na kujenga miundombinu ya kitalii, kufanya shughuli za kitalii na kupitia uwekezaji huo,serikali imekuwa ikipata mapato mbali mbali yanayojumuisha ada za vitalu,tozo za wanyama wanaowindwa,malipo ya vibali vya uwindaji wa kitalii na malipo ya watalii wasindikizaji.

 

Ameweka bayana kwamba Tawa kanda ya kati pia inasimamia vitalu vya uwindaji wa kitalii vilivyopo kwenye maeneo ya wazi vya Rungwa kaskazini pamoja na Rungwa kusini ambapo katika kipindi cha miaka mitatu ya 2022/2023 hadi 2024/2025 serikali kupitia Tawa Kanda ya kati imeingiza takribani shilingi bilioni 12,657,626,387.60 kupitia shughuli za utalii zinazofanyika katika mapori ya Akiba Rungwa Kizigo na Muhesi.

 

Akizungumzia wanyamapori,wakali na waharibifu,Kamanda huyo wa Tawa Kanda ya kati hata ameweka bayana kuwa kanda ya kati inakabiliwa na changamoto kubwa ya uwepo wa matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo ya wilaya mbali mbali za Mkoa wa Singida.

 

Ameyata maeneo mengine yenye changamoto kuwa ni pamoja na wilaya ya Manyoni,Ikungi,Mkalama,Singida vijijini,Singida mjini pamoja na wilaya ya Iramba na kwamba kazi za kudhibiti wanyamapori wakali,waharibifu kwenye maeneo mbali mbali ya vijiji vilivyopo katika wilaya hizo,imeweza kuokoa maisha ya wananchi na mali zao kama vile mazao,mifugo,makazi na uwindaji haramu wa wanyamapori.

 

Katika kuhakikisha usalama wa wananchi na mali zao,Kamishina Nyanda amesema ofisi ya Kanda pamoja na Mapori ya Akiba kwa kushirikiana na Halmashauri za wilaya husika wamekuwa wakifanya doria za kuzuia wanyamapori wakali  na waharibifu kwa kushirikiana na askari wa akiba wa vijiji katika wilaya husika

MWISHO.

Post a Comment

Previous Post Next Post