KIKWETE AHIMIZA USHIRIKI WA WATUMISHI KWENYE MICHEZO

 Na Mwandishi Wetu, Singida

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Ridhiwani Kikwete amewakumbusha viongozi wa mashirika, taasisi,  idara na ofisi za serikali kuhusu umuhimu wa kushirikisha watumishi kushiriki kwenye michezo mbalimbali ikiwemo ya mashirikisho pamoja na Mei Mosi.


Mhe. Ridhiwan amesema michezo sio kwamba imetengenezwa ili watumishi waende kustarehe nje ya vituo vya kazi bali lengo la michezo hii kuimarisha afya na utimamu wao, ili wanaporejea makazini waendelee kutoa tija.


“Napenda kuwakumbusha viongozi na mimi nikiwa Waziri ninayesimamia eneo hili, kuendelea kutambua kuwa serikali ya Awamu ya Sita itaendelea kuimarisha utimamu wa watumishi wa umma kupitia michezo, hivyo ni wajibu wao kama wasimamizi wa ofisi zao kuendelea kuwapa ruhusa wanamichezo   kushiriki, ili kuimarisha afya zao na utimamu wao na hata wanaporudi makazini wawe na afya njema zaidi,” amesema Mhe. Ridhiwani 



Wakati akimnukuu Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Doto Biteko wakati akifunga michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala za Serikali na Ofisi za Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI) iliyofanyika mwaka 2024  mkoani Morogoro “aliwakumbusha viongozi, wakuu wa taasisi na Idara kuhakikisha kuwa wafanyakazi washiriki kwenye michezo hii ikiwa ni sehemu ya kuimarisha afya zao lakini pia kuimarisha mahusiano haya”. 


Mhe. Ridhiwan amewapongeza Kamati ya Michezo ya Kombe la Mei Mosi pamoja na TUCTA kwa kuandaa michuano bora, amewapongeza pia washiriki wote kwa kutoa burudani kwa kushinda na kutunza afya zao.


Hatahivyo, amewataka watumishi kuendeleza michezo mahala pa kazi ili kuimarisha afya zao. 



Halikadhalika ameipongeza huduma ya afya kwa kutoa wahudumu na magari ya wagonjwa kwa viwanja vyote.


“Michezo sio burudani pekee bali ni sehemu muhimu husaidia kuimarisha afya, mahusiano na kuongeza tija mahala pa kazi, ambapo inakwenda sambamba na kaulimbiu ya michezo kwa afya, dhima furaha mahala pa kazi inaendelea wafanyakazi tiushiriki vyema uchaguzi 2025 tupate viongozi wazuri na wema kwa ushirikiano mzuri,” amesema Mhe. Ridhiwan.  


Katika hatua nyingine, amehimiza watumishi wa umma kushiriki ipasavyo katika uchaguzi mkuu wa 2025 ili kuchagua viongozi bora kwa kuangalia maslahi mapana ya nchi, na kujenga umoja wa nchi yetu, na kuendelea kuenzi amani ya nchi kama ilivyokuwa ndoto za wazee na waasisi wa nchi hii.


Amempongeza na kumshukuru Mhe.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuuwekazi mkubwa alioweka kwenye michezo na afya kwa kujenga miundombinu ya viwanja vya bora na  kisasa, ambapo wamedhamiria kuimarisha sekta ya michezo.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya michezo ya Mei Mosi, Bi. Roselyne Massam amesema michezo hii imepata changamoto ya kupungua kwa timu shiriki kutoka 54 za mwaka jana hadi 44 za mwaka huu 2025, kutokana na wakuu wengi kutoona umuhimu wa michezo hii na kutoruhusu watumishi wao kushiriki.


Amewataka watumishi kuendelea kufanya mazoezi kila wakatoi na sio kusubiri michezo ili kuimarisha afya zao na kuongeza tija mahala pa kazi.



Bi. Roselyne ameipongeza serikali kwa kuipa kipaumbele michezo kwa kuboresha miundombinu ya michezo na kuongeza hamasa zaidi katika michezo.


Ameishukuru Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kusimamia vyema michezo na kuhakikisha inafanyika kila mahali.


Amesema michezo iliyoshindaniwa ni mpira wa miguu, netiboli, wavu, kikapu, baiskeli, riadha, karata, bao, darts, draft na kuvuta kamba


MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post