Na. Sylvester Richard
Wananchi wa Mkoa wa Singida wametakiwa kuongeza juhudi katika kufanya usafi wa mazingira ili kulinda afya zao katokana na magonjwa ya mlipuko yatokanayo na uchafu.
Hayo yamebainishwa Juni 19, 2024 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Amon Daudi Kakwale alipokuwa anaongea na wananchi wakiwemo wafanyabiashara waliopo soko kuu la Manispaa ya Singida.Aidha, SACP Kakwale aliyefika sokoni akiongoza askari kwenye zoezi la kufanya usafi kufuatia wiki ya Utumishi wa Umma ambayo huanza kila ifikapo Juni 16, na kufikia kilele chake tarehe 23 mwezi huo Kila mwaka, amesema kufanya usafi itaepusha magonjwa mbalimbali ambayo ni pamoja na magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu, kuharisha na kuhara damu.
Ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuongeza ushirikiano na Jeshi la Polisi katika kuimarisha usalama wa raia na mali zao kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu zitakazosaidia kuwabaini, kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani ili kuufanya Mkoa wa Singida kuwa imara zaidi katika ulinzi na usalama.
Naye, Theresia John, Afisa Mazingira Manispaa ya Singida, amelishukuru Jeshi la Polisi kwa kufanya usafi kwani vyakula vinapaswa kuuzwa katika eneo safi kuwasisitiza wafanyabiashara wa soko hilo kufanya usafi bila kushurtishwa bali iwe ni tabia endelevu ili soko liwe safi wakati wote.
Akiongea kwa niaba ya wafanyabiashara wa soko hilo, Bw. John Mwashinjala ambaye ni Katibu wa Umoja wa wafanyabiashara soko kuu la Singida, ameeleza kuwa wao kama wafanyabiashara wamefurahishwa na kushangazwa na zoezi hili kwani hawakulitarajia na kuwataka wananchi kutowaogopa askari wa Jeshi la Polisi bali wawaone kama kimbilio lao kwa sababu wanashirikiana na kuwalinda raia na mali zao.
hongera Sana mwamba
ReplyDeleteShukran Katibu
Delete