Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA
SERIKALI Mkoa wa Singida
imewataka watumishi wa umma na watu binafsi kutumia Mfumo wa Anwani za Makazi
(NaPA) katika kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwa unarahisisha utoaji na
ufikishaji wa huduma kwa urahisi na kuondoa usumbufu wa kutumia gharama kufika katika
ofisi za Serikali.
Mkuu wa Wilaya ya Singida,Godwin
Gondwe, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema
hayo jana wakati akifunga mafunzo kuhusu anwani za makazi kwa watumishi wa
serikali,taasisi binafsi na viongozi wa dini yaliyofanyika kwenye ukumbi wa
ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida.
"Kila mfanyakazi wa serikali
ambaye unajua kwamba unatoa huduma kwa wananchi ni muhimu sana na ni wajibu
kupakua app ya NaPA ili kuweza kurahisisha kufikisha huduma kwa wananchi,"
alisema
Gondwe alisema suala la Mfumo wa Anwani za Makazi (NaPA) linatakiwa
kuchukuliwa kwa umuhimu wa kipekee sana kwani itafika wakati mtu anaweza kupata
huduma serikalini au sehemu yeyote akiwa
nyumbani kwake kwa kuingia kwenye mtandao wa NapA.
"Sisi kama viongozi wa
serikali tunatakiwa kutoa huduma kwa wananchi kwa kutumia mfumo wa NaPA na
mtakumbuka Rais Samia Suluhu Hassan amezengumzia sana kutatua kero na
changamoto za wananchi na ametoa minara ili tuweze kuwahudumia wananchi kwa
haraka kwani hivi sasa dunia inakwenda kwa kasi sana," alisema Gondwe.
Alisema serikali imetengeneza
mfumo wa NaPA ili kurahisisha huduma kwa
wananchi hivyo unamhusu kila ambaye anafanya kazi serikali na asiye kwenye
taasisi za serikali ambapo kwa watendaji wa kata mfumo huo utasaidia kupunguza
siku za wananchi kupata huduma katika ofisi za kata.
"Tunafahamu sana mitandao ya
kijamii kama vile Instagram,Tiktok ndio kama ilivyo NaPA na hii ni 'app' au
'soft ware' ambazo zimekuja kurahisisha huduma kwa watu mbalimbali hivyo
tunaweza kusema tumetengenewa sehemu ya kukutana mtandaoni ili kupata huduma na
wananchi kuhudumiwa haraka," alisema Gondwe.
Mkuu huyo wa Wilaya ameongeza kuwa uzuri wa mfumo huu ni kwamba
unakuwa ni rahisi kurejea kumbukumbu badala ya ngoja niende kwenye 'file' lakini kupitia mfumo huu mtu anabofya tu
matokeo yanatokea moja kwa moja.
Gondwe alisema wafanyabiashara
wanaofanya biashara zao mitandaoni itawarahisishia sana kuweza kufikisha bidhaa
zao kwa wateja kirahisi na kuwajua wateja wao walipo.
"Badala ya kumwelekeza mtu
kata kulia eeh hapa hapa angalia mti wa mbuyu kumbe mbuyu ulishakatwa zamani au
angalia nyumba ya rangi ya kijani kumbe rangi ilishabadilishwa zamani,lakini
kwa kutumia mfumo wa NaPA usumbufu wa kuelekeza hivyo hautakuwepo kwa kuwa mtu
ataweza kuingia kwenye mfumo na kufika eneo husika kwa urahisi," alisema.
Alisema kutokana na umuhimu
mkubwa wa Mfumo wa Anwani za Makazi kila mtumishi wa serikali na wananchi kwa
ujumla wapakue 'app' ya NapA katika simu yake janja.
"Kwa maafisa Utumishi kwasababu
serikali inatumia nyaraka za kielektroniki mtumishi anapohamishwa kupelekwa
kituo kingine cha kazi wawe wanakabidhi pia nyaraka za kielektroniki ili
kutowachanganya wananchi wanapokuwa wanapata huduma kupitia mfumo wa
NaPA," alisema.
Naye Mratibu Msaidizi w Anwani za
Makazi Kitaifa kutoka Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Arnold
Mkude,amesema katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kumeanzishwa
utaratibu wa utoaji wa barua ya utambulisho lengo ikiwa ni kuendana na kasi ya
ukuaji wa uchumi wa kidigitali.
Alisema hatua iliyofikiwa ya
utoaji wa barua ya utambulisho ni kwamba majaribio yameanza kufanyika kuanzia
mwezi Machi hadi Mei 2024 ambapo wadau katika suala hilo ni watendaji wa
kata,mitaa,vijiji,watoa huduma na wananchi na lengo la majaribio hayo ni kubainisha
mapungufu na changamoto ili kuboresha kabla ya kuanza matumizi nchi nzima.
Mkude alisema tangu operesheni
Anwani za Makazi ianze zimeweza kukusanywa taarifa za Anwani za Makazi milioni
12. 8 na zimewekwa nguzo za majina ya barabara zaidi 222,000 na vibao vya namba
za nyumba zaidi ya milioni 4.
Alisema shughuli kuu
zinazofanyika katika utekelezaji wa mfumo wa NaPA ni kusajili majina ya
barabara na kutoa namba za Anwani za Makazi,kukusanya na kuhuisha taarifa za
Anwani za Makazi,kuweka miundombinu ya mfumo,kutoa elimu na kuwajengea uwezo
kwa watekelezaji na watumiaji wa mfumo.
"Kuna manufaa makubwa ambayo
yamepatikana tangu kuanza kwa Mfumo wa Anwani za Makazi kwa mfano kwa Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA) matumizi yalipoanza Aprili 2023 katika suala la
kukusanya kodi ya majengo kumesaidia kuongeza idadi ya maghorofa kutoka 4,164
hadi kufikia 32,000 na majengo ya kawaida kufikia 5,117,050 kutoka 2,988,546
yaliyokuwa yanatambulika awali kabla ya kuanza kwa mfumo huo.
Naye Mtaalamu wa Mfumo wa Anwani ya
Makazi kutoka Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Innocent
Jacob, alisisitiza wananchi kuhakiki
anwani zao na kutumia program tumizi ya umma (NaPA) kujua anwani zao
kwani anwani za makazi ni fursa katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Mratibu wa Kitaifa wa Utekelezaji
wa Mfumo wa Anwani ya Makazi kutoka Wizara ya Habari,Mawasiliano na Teknolojia
ya Habari, Mhandisi Jampyoni Mbugi amesema utumiaji wa mfumo huo utasaidia sana
utoaji wa huduma na kuondoa matukio ya kiuhalifu kwa kuwa kila mtu atajulikana
alipo.
Naye Afisa Tehama, George
Leonard, alisema utaratibu wa utoaji wa barua za utambulisho utawarahisishia
wananchi kupata huduma kwa njia ya mtandao.
Nao washiriki wa mafunzo hayo
waliitaka serikali kuendelea kutoa elimu zaidi kwa wananchi kuhusu umuhimu wa
Mfumo wa Anwani za Makazi ili waweze kuwa na uelewa mkubwa na kuutumia katika
kupata huduma kwenye taasisi za serikali na zisizo za serikali.
MWISHO


Post a Comment