Na Sylvester Richard
Madereva wa vyombo vya usafiri mkoani Singida wamehimizwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa pikipiki na magari yao ili kubaini mapema hitilafu zinazoweza kusababisha ajali barabarani.
Rai hiyo imetolewa na Sajenti wa Polisi Mashaka Zacharia wakati akitoa elimu ya usalama barabarani kwa wananchi kupitia Standard Radio Singida Agosti 13, 2026.
Sajenti Mashaka amesema madereva na wamiliki wa vyombo vya usafiri wanapaswa kuzingatia sheria kwa kuhakikisha vyombo vyao vinakaguliwa na kurekebishwa kabla ya kuvipeleka kwa Afisa Mkaguzi wa Magari wa Kitengo cha Usalama Barabarani.
Amesema ukaguzi wa mara kwa mara ni muhimu kwa sababu unasaidia kubaini mapema matatizo ya kiufundi ambayo yanaweza kuhatarisha maisha ya dereva, abiria na watumiaji wengine wa barabara.
Kuhusu bima, amewataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuhakikisha bima zao zinafanyiwa upya kwa wakati zinapomalizika ili kuepuka hatua za kisheria, ikiwemo kulipa faini au kufikishwa mahakamani.
Aidha, amewahimiza madereva kufika katika ofisi za Wakuu wa Usalama Barabarani kwa ajili ya ukaguzi wa hiari na kupata msaada kuhusu stika za usalama barabarani kwa wakati.


Post a Comment