YAGI KIARATU - RAIS KWA UNYENYEKEVU MKUBWA TUNAOMBA UTUJENGEE SOKO JIPYA SINGIDA MJINI


Na Thobias Mwanakatwe, SINGIDA

MGOMBEA Ubunge Jimbo la Singida Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yagi Kiaratu, amewasilisha ombi kwa mgombea urais wa chama hicho, Dk.Samia Suluhu Hassan la kujengewa soko jipya mjini Singida kwa kuwa lililopo limechakaa na linahatarisha usalama wa wananchi na wafanyabiashara.


Amewasilisha ombi hilo leo wakati akizungumza na mamia ya wananchi kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Bombadia Manispaa ya Singida ambalo uliandaliwa maalum kwa ajili ya mgombea urais CCM Dk.Samia kunadi sera na ilani ya CCM.


“Wazee wameninong’oneza hapa mji wa Singida tuna soko kongwe sana ambalo linatishia usalama wa walaji na wafanyabiashara, soko hilo limejengwa tangu 1958 limechakaa na ni kongwe, mheshimiwa rais kwa unyenyekevu mkubwa wananchi wa Singida wanaomba uwajengee soko jipya,”amesema Kiaratu na kushangiliwa na wananchi wa Manispaa ya Singida.



“Mheshimiwa mgombea wetu imani inalipwa kwa imani, umetuonesha imani kubwa na sisi watu wa Singida tutakulipa kwa imani kubwa kutokana na mambo makubwa uliyotufanyia na utaiona Imani yetu Oktoba 29 kwa wananchi waliojiandikisha kupiga kura hakika watakupa kura za kishindo,” amesema Kiaratu.


Kiaratu amesema kwa kipindi cha awamu tatu amekuwa diwani na mstahiki meya wa Manispaa ya Singida hivyo anaifahamu Singida ilikotoka na iliyopo sasa na hivyo amekuwa shuhuda namba moja kwa kazi kubwa alizofanya rais Dk.samia licha ya kwamba alichukua nchi katika kipindi kigumu cha kumpoteza rais aliyekuwa madarakani.



“Jimbo la Singida mjini limepokea fedha nyingi sana, umemimina pesa wala hukudondosha, tumejenga mashule, madarasa tumepata walimu, Halmashauri ya Manispaa ya Singida ilikuwa haina Hospitali ya Wilaya lakini leo ipo, tuna jengo zuri la dharula, tuna jengo la mama na mtoto ambalo mama mjamzito akiingia hapo anatoka na mtoto,”amesema Kiaratu.


Singida mjini pia ilikuwa na shida ya maji, tumepata mradi mkubwa wa miji 28 wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 42, hivi sasa wataalam wanatafuta vyanzo vya maji na kwa fununu visima vitatu vimeonesha dalili za kutoa maji mengi na hiyo inaenda kuwa mwarobaini wa shida ya maji.

 


Singida ni mji unaokuwa haraka tuna shida ya barabara na mitandao ya lami mjini, lakini mwaka huu tumepata mradi mkubwa wa TACTIC tunakwenda kujenga kilometa saba za lami, tunajenga soko kubwa la vitunguu na tunakwenda kutibu korongo kubwa la Minga ambalo imekuwa changamoto kwa wananchi.


“Watu wa singida wanataka kuithibitishia dunia kwamba kupiga kura ni haki ya kikatiba ,sote tunakwenda kupiga kura tutakuchagua wewe, tutawachagua wabunge wa majimbo nane ya Singida na madiwani wa kata 136 za mkoa wa Singida. Singida tuna imani na wewe tutakwenda kupiga kura na chachu kubwa ni ilani uliyoitengeneza safari hii, mtu wa Singida unamwambia unakwenda kujenga kiwanja cha ndege, kutuletea SGR na barabara.


MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post