TCRA YAPEWA KONGOLE KWA UFADHILI MASHINDANO YA KIMATAIFA YA HISABATI

 

Na Thobias Mwanakatwe,SINGIDA 



CHAMA cha Hisabati Tanzania (MAT/CHAHITA) kimeishukru Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa jinsi ambavyo imekuwa msaada mkubwa katika   kuwezesha mashindano ya kimataifa ya Hisabati na kuwezesha Tanzania kupata ushindi katika mashindano ya Afrika (PAMO).


Mwenyekiti wa Chama hicho, Dk. Said Sima, alitoa pongezi hizo jana wakati akitoa matokeo ya mashindano ya kitaifa (TAMO) ya Hisabati kwenye mkutano mkuu wa chama ambao pia ulikwenda sambamba na kutoa mafunzo kwa walimu wa Hisabati kutoka mikoa yote nchini.



Dk.Sima amesema kutokana na ufadhili wanaoupata kutoka TCRA na wadau wengine umekiwezesha chama hicho kushinda   mashindano ya Afrika (PAMO) kwa mwaka 2024 na 2025 nchini Afrika Kusini na Botswana kwa kutwaa medali nne za shaba kila mwaka.


"Kwanza tunatoa shukrani nyingi sana kwa wafadhili waliowezesha Shuguli za mashindano ya kimataifa na zawadi kwa washindi wa kitaifa wa mwaka jana,wafadhili hawa ni TCRA,UDSM,BARRICK Tanzania na Benki ya CRDB," alisema Dk.Sima.



Dk.Sima alisema MAT/CHAHITA  kinaziomba taasisi nyingine kujitokeza kutoa motisha kwa washindi ikiwa ni sehemu ya kuendeleza vipaji na kuunga mkono juhudi za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan katika kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini.


Naye Afisa Elimu Mkoa wa Singida Dk.Elpidius Baganda,alisema kwa sasa walimu wajikite katika kuwafundisha wanafunzi kujiajiri wanapohitimu masomo kwasababu ajira serikalini zimepungua.


Dk.Baganda alisema mafunzo kwa walimu wa hisabati yamekuja wakati mwafaka ambapo serikali imejenga shule nyingi za amali ambazo zitahitaji sana hisabati.


Awali akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk. Jabir Bakari, Meneja wa Mamlaka hiyo Kanda ya Kati-Dodoma, Asajile John, alikitaka chama hicho  kushirikiana na shule na halmashauri nchini kuanzisha na kuimarisha Klabu za Hisabati na za kidigitali shuleni na kuondoa dhana potofu somo hilo la Hisabati haliwezekaniki


Asajile, alisema TCRA inatambua umuhimu mkubwa wa Hisabati na kwamba jamii imejenga dhana potofu ya kuwa haliwezekani kutokana na kuwa somo lina changamoto nyingi katika ufundishaji na ujifunzaji ngazi zote za elimu.


“Kupitia MAT/CHAHITA mna nafasi nzuri ya kuendelea kufuta dhana potofu juu ya somo la Hisabati kwa vitendo kwa kupeana uzoefu wenye lengo la kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa somo hili katika shule zetu na kubadilishana uzoefu katika mada zenye changamoto za ufundishaji na ujifunzaji,” alisema. 


MWISHO

Post a Comment

Previous Post Next Post